Michezo

Kenya yataja kikosi cha Kombe la Dunia Kriketi

February 18th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA watetezi Kenya wametaja kikosi cha wachezaji 14 kitakachowania tiketi ya kuingia Kombe la Dunia la Kriketi kutoka mashindano ya daraja ya kwanza ya Bara Afrika kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 19 yatakayofanyika mjini Windhoek, Namibia mnamo Machi 15-24, 2019.

Kenya watakabiliana na Uganda, Tanzania, Namibia, Sierra Leone na Nigeria katika mashindano hayo ya mataifa sita ambayo mshindi pekee ataingia Kombe la Dunia litakaloandaliwa nchini Afrika Kusini mwaka 2020.

Timu ya Kenya iliibuka bingwa wa Afrika mwaka 2017 baada ya kumaliza juu ya jedwali la mashindano ya mzunguko yaliyowakutanisha dhidi ya Uganda, Ghana na Botswana na kushiriki Kombe la Dunia nchini New Zealand. Ilimaliza Kombe la Dunia katika nafasi ya 15 kati ya mataifa 16 yaliyoshiriki baada ya kulemea Papua New Guinea iliyovuta mkia.

Sukhdeep Singh, ambaye ni mchezaji wa Kenya aliyesalia katika kikosi kilichoshinda ubingwa wa Afrika mwaka 2017 na kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2018, ametwikwa majukumu ya nahodha.

Kikosi cha Kenya: Sukhdeep Singh (nahodha), Shukan Mehta, Sukhraj Singh, Brij Patel, Dilan Shah, Shay Shah, Krushil Savla, Hashit Vekaria, Francis Mutua, Vraj Patel, Pradyuman Joshi, Jairaj Pujara, David Okaro, Satish Hirani.