Michezo

Kenya yateremka kwenye uorodheshaji wa Fifa

July 25th, 2019 4 min read

Na GEOFFREY ANENE na CHRIS ADUNGO

TIMU ya taifa ya Kenya almaarufu Harambee Stars imeteremka nafasi mbili hadi nambari 107 katika viwango vipya vya ubora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Katika viwango hivyo vya mataifa 211 vilivyotangazwa Julai 25, vijana wa kocha Sebastien Migne, ambao walikuwa wameruka juu nafasi tatu hadi nambari 105 duniani Juni 14, wamepoteza alama sita. Wakenya sasa wana jumla ya alama 1201.

Kuanguka kwa Kenya katika viwango hivi kulichangiwa na wao kuwa na kampeni ya kusikitisha kwenye Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri kati ya Juni 21 na Julai 19 walipobanduliwa nje katika mechi za makundi baada ya kubwagwa 2-0 na Algeria na 3-0 na Senegal, ambazo zilimaliza mashindano haya katika nafasi ya kwanza na pili mtawalia, na kuchapa Tanzania 3-2 katika mechi za Kundi C.

Senegal bado ni namba wani barani Afrika baada ya kuruka juu nafasi mbili hadi nambari 20 duniani. Teranga Lions inafuatiwa na Tunisia ambayo kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Senegal katika nusu-fainali kimechangia wao kuteremka nafasi nne hadi nambari 29 duniani.

Washindi wa medali ya shaba Nigeria wameimarika kwa nafasi 12 hadi nambari 33 duniani. Algeria ya kocha Djamel Belmadi ndiyo timu iliyofanya vyema zaidi katika viwango hivi baada ya kupaa nafasi 28 na kutulia katika nafasi ya 40 duniani.

Morocco na Misri ambayo ilikuwa mwenyeji wa AFCON 2019, zimepanda nafasi sita na tisa mtawalia hadi nambari 41 na 49 duniani.

Ghana haijasonga kutoka nafasi ya 50 duniani. Cameroon, ambayo ilitetea ubingwa wa Afrika bila mafanikio, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimeshuka nafasi mbili na saba mtawalia. Zinashikilia nafasi ya 53 na 56, mtawalia.

Ivory Coast (nafasi tano juu hadi nambari 57 duniani) inakamilisha orodha ya timu 10-bora barani Afrika.

Katika nafasi ya 80 duniani, Uganda ndiyo nambari moja katika eneo la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa). Waganda wamekwamilia nafasi hiyo. Wanafuatiwa na Wakenya katika nafasi ya 107 kutoka 105, Sudan wako juu nafasi moja hadi 129 nao Rwanda wamepaa nafasi tatu hadi 133.

Tanzania ambao walirejea katika AFCON kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980, wametupwa chini nafasi sita hadi 137 duniani.

Watanzania wanatarajiwa kualika Harambee Stars kwa mechi ya kufuzu kushiriki soka ya wachezaji wanaosakata katika mataifa yao almaarufu CHAN mnamo Julai 28 jijini Dar es Salaam. Walipoteza mechi zao zote nchini Misri dhidi ya Senegal (2-0), Kenya (3-2) na Algeria (3-0).

Burundi, ambayo iliingia AFCON kwa mara ya kwanza kabisa mwaka 2019, imeporomoka kwa nafasi 14 hadi nambari 148 duniani. Haikufunga bao katika vichapo vya mabao ya kufanana ya 1-0 ilivyopokea dhidi ya Nigeria na Madagascar (1-0) na pia ikalimwa 2-0 na Guinea katika mechi za makundi.

Ethiopia inasalia katika nafasi ya 150 duniani. Sudan Kusini imeshuka nafasi moja hadi nambari 169 duniani. Djibouti, Somalia na Eritrea ziko katika nafasi tatu za mwisho duniani.

Kuna mabadiliko makubwa katika orodha ya timu 10 za kwanza duniani. Ubelgiji inasalia ya kwanza.

Inafuatiwa na Brazil. Mabingwa wapya wa Copa Amerika, Brazil, wameondoa Ufaransa katika nafasi ya pili.

Wafalme wa Kombe la Dunia Ufaransa wako katika nafasi ya tatu. Uingereza haijasonga kutoka nafasi ya nne. Uruguay imeimarika kwa nafasi tatu hadi nambari tano.

Kuimarika kwa Uruguay kumesukuma chini washindi wa Ligi ya Bara Ulaya Ureno na wanafainali wa Kombe la Dunia Croatia wameshuka nafasi moja kila mmoja hadi nambari sita na saba mtawalia.

Colombia imepaa nafasi tano hadi nambari nane. Uhispania na Argentina zinashikilia nafasi za tisa na kumi baada ya kuteremka nafasi mbili na kupanda moja, mtawalia.

Kuteremka kwa Kenya katika viwango vya wanaume kunawasili siku chache baada ya kinadada wao (Harambee Starlets) pia kufanya vibaya katika viwango vya wanawake. Starlets ya kocha David Ouma ilishuka nafasi tatu hadi nambari 141 duniani katika viwango vilivyotangazwa Julai 12.

Starlets inajiandaa kwa mechi za kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki mwaka 2020 dhidi ya Malawi mwezi Agosti.

Kenya imani tele itatoa ‘Pharaohs’ kamasi Afcon ’21

Harambee Stars watafungua kampeni zao za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021 dhidi ya Misri ugenini kisha Kupiga mchuano wao wa mwisho wa Kundi G dhidi ya Togo jijini Lome.

Stars wamo katika zizi moja na Togo, Comoro Islands na Misri waliokuwa wenyeji wa fainali za AFCON 2019.

Fainali za AFCON 2021 ambazo pia zitajumuisha jumla ya vikosi 24, zitaandaliwa na Cameroon ambao awali, walikuwa wawe wenyeji wa fainali za 2019.

Hata hivyo, mwendo wao wa kobe katika kufanikisha maandalizi ya kivumbi hicho uliwachochea vinara wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kuwapokonya haki na idhini ya kuwa waandalizi.

Baada ya kuvaana na ‘The Pharaohs’ ya Misri mnamo Novemba mwaka huu, Stars watapimana ubabe na Togo katika uwanja wa MISC Kasarani, Nairobi.

Katika mchuano wa tatu, Kenya itapepetana na Comoro mbele ya mashabiki wao wa nyumbani jijini Nairobi kabla ya kurudiana na kikosi hicho katika mechi yao ya nne.

Chini ya kocha Sebastien Migne, Stars watamenyana baadaye na Misri kati ya Oktoba 5-13 kisha kusafiri Lome kuvaana na Togo kati ya Novemba 9-17.Mechi za raundi ya kwanza na pili zitasakatwa kati ya Novemba 11-19 huku michuano ya raundi za tatu nan ne zikiratibiwa kusakatwa kati ya Agosti 31 na Septemba 8 mwaka ujao. Licha ya Stars kutiwa katika hilo kundi gumu, Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa ni mwingi wa matumaini kwamba kikosi hicho kitajikakamua vilivyo na kufuzu kwa fainali za AFCON kwa mara ya pili mfululizo.

“Tuna nafasi nyingine ya kufuzu kwa fainali za AFCON. Kikubwa zaidi kinachohitajiwa na Stars ni kusajili ushindi katika michuano yote ya nyumbani na kujivunia angalau sare moja ugenini,” akasema Mwendwa.

Kenya walioshiriki fainali za AFCON 2019 baada ya kuwa nje kwa kipindi cha miaka 15, walibanduliwa mapema kwenye hatua ya makundi.

Katika kipute hicho, Kenya waliopangwa katika Kundi C, walisajili ushindi mmoja pekee dhidi ya Tanzania huku wakizidiwa maarifa na Algeria na Senegal ambao baadaye walikutana kwenye fainali iliyowashuhudia Desert Foxes kutoka Algeria wakitawazwa wafalme kwa mara ya kwanza tangu 1990.

Mara ya mwisho kwa Kenya kushiriki makala ya mashindano ya AFCON yakifuatana ni katika miaka ya 1988, 1990 na 1992.

Stars walifuzu kwa fainali za AFCON kwa mara ya kwanza mnamo 1972. Japo Kenya wana uwezo wa kuwakomoa Comoros, mtihani wao mgumu zaidi ni jinsi ya kuwazidi maarifa Togo na Misri ambao ni mabingwa mara saba wa taji la AFCON.

Katika jumla ya mechi 19 kuwahi kuwakutanisha Kenya na Misri, Stars wameibuka na ushindi mara moja pekee katika matokeo ya 3-1 mnamo 1979.

Mechi nne zimeishia sare, huku Misri wakiwapepeta Kenya katika jumla ya michuano 14 zikiwemo tano zilizopita ambazo zilikuwa za kirafiki.

Misri inayojivunia huduma za mvamizi mahiri wa Liverpool, Mohamed Salah, pia ina rekodi nzuri dhidi ya Togo.

Misri wanajivunia kuwalaza Togo mara sita, kusajili sare moja na kupokezwa kichapo mara moja.

Kutokana na rekodi duni ambayo Kenya na Togo wanayo dhidi ya Pharaohs, Misri wanapigiwa upatu wa kuibuka kileleni mwa Kundi G. Vita vya kuwania tiketi nyingine moja ya kufuzu kwa AFCON 2021 kutoka Kundi G vinasalia kuwa kati ya Kenya, Togo na Comoros ambao hawajawahi kunogesha fainali za kivumbi hiki.