Michezo

Kenya yateremka kwenye uorodheshaji wa viwango bora Fifa

October 24th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA ndiyo nchi ya pekee kutoka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ilioteremka kwenye viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) vilivyotangazwa Alhamisi.

Harambee Stars ya kocha Francis Kimanzi ilizabwa 1-0 na wageni wake Msumbiji katika mechi ya kirafiki uwanjani Kasarani mnamo Oktoba 13.

Imeshuka kutoka 107 hadi nambari 108. Alama za Kenya pia zimepungua kutoka 1201 na kuwa 1195.

Uganda inasalia nambari moja Cecafa.

Uganda Cranes imepaa juu nafasi moja hadi nambari 79 duniani.

Walilima Ethiopia 1-0 Oktoba 13 katika mechi ya kirafiki na kupepeta Burundi 3-0 mnamo Oktoba 19 na kuingia soka ya Bara Afrika ya wachezaji wanaosakata katika mataifa yao almaarufu CHAN 2020.

Taifa linalofuata Uganda katika Cecafa ni Kenya katika nafasi ya 108 duniani baada ya kuteremka nafasi moja. Sudan imekwamilia nafasi ya 128 duniani ikifuatiwa na Rwanda (nafasi moja juu hadi 129 duniani) na Tanzania (imeimarika kutoka 135 hadi 133 duniani).

Burundi imepaa kutoka 144 hadi 143, Ethiopia inasalia nambari 151, huku Sudan Kusini ikishikilia taji la timu ilioimarika zaidi mwezi huu, kwa pamoja na Nicaragua ya eneo la Caribbean, baada ya kuruka nafasi 11 na kutulia katika nafasi ya 162. Djibouti, Somalia na Eritrea zimepiga hatua moja mbele hadi nambari 185, 198 na 206, mtawalia.

Mataifa yanayoshikilia nafasi 10 za kwanza barani Afrika ni Senegal (haijasonga kutoka 20 duniani), Tunisia (imekwamilia 29), Nigeria (iko chini nafasi moja hadi nambari 35 duniani), mabingwa wa Afrika Algeria (wamesalia katika nafasi ya 38 duniani), Morocco (imeshuka nafasi tatu hadi nambari 42 nazo Misri na Ghana zinapatikana katika nafasi za 49 na 51, mtawalia.

Cameroon na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimeruka juu nafasi moja. Zinapatikana katika nafasi za 52 na 54, mtawalia. Ivory Coast inakamilisha orodha ya mataifa 10-bora barani Afrika katika nafasi ya 56 duniani.

Msumbiji yasalia pale pale

Msumbiji, ambayo iliaibisha Kenya 1-0 mbele ya mashabiki wake uwanjani Kasarani, imesalia katika nafasi ya 112 duniani.

Togo, ambayo Kenya itaalika hapo Novemba 19 kwa mechi ya pili ya Kundi G ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) la mwaka 2021, imekwamilia nafasi ya 124.

Wanavisiwa wa Comoros pia wanapatikana katika kundi hili, ambalo pia lina Misri, wameimarika kutoka 147 hadi 142 duniani. Comoros ilishangaza Guinea 1-0 katika mechi ya kujipima nguvu mnamo Oktoba 12 nchini Ufaransa.

Kenya itaanza kampeni ya kutafuta tiketi ya kuwa katika Afcon mwaka 2021 dhidi ya miamba Misri mnamo Novemba 11 kabla ya kukaribisha Togo.

Hakuna mabadiliko katika nafasi nne za kwanza duniani ambazo zinashikiliwa na Ubelgiji, Ufaransa, Brazil na Uingereza katika usanjari huo. Uruguay imerukia nafasi ya tano baada ya kubadilishana nafasi ya sita na Ureno. Croatia pia imepaa nafasi moja hadi nambari saba na kusukuma Uhispania nafasi moja chini hadi nambari nane. Argentina imerukia nafasi ya tisa baada ya kung’oa Colombia kutoka nafasi hiyo. Colombia ndio inafunga mduara wa 10-bora duniani. Uholanzi iko juu nafasi moja hadi nambari 12. Italia na Ujerumani zinasalia katika nafasi za 15 na 16 duniani, mtawalia.