Habari

Kenya yatoka sare ya 1-1 dhidi ya wenyeji Misri

November 15th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MICHAEL Olunga alisaidia Harambee Stars kuzoa alama moja muhimu Alhamisi usiku katika mechi ya ufunguzi ya Kenya ya Kundi G ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (Afcon) mwaka 2021 aliposawazisha 1-1 uwanjani Borg El Arab mjini Alexandria, Misri.

Kenya iliingia mchuano huo bila ushindi dhidi ya Misri katika mechi 15 mfululizo. Misri iliyokosa mshambuliaji matata Mohamed Salah anayeuguza jeraha, iliona lango dakika ya 42 baada ya Mahmoud Kahraba kuiba pasi mbovu kwa kipa.

Vijana wa kocha Francis Kimanzi, ambao waliingia mechi hii bila ushindi baada ya kulimwa 1-0 na Msumbiji na kukabwa 1-1 na Uganda katika mechi za kujipima nguvu, ilihangaishwa sana katika kipindi cha kwanza.

Katika kipindi hicho, Kahraba na Ahmed Hegazi walipata nafasi kadhaa nzuri. Hata hivyo, Eric Johana Omondi alimlazimu kipa Mohammed Elshenawy kufanya kazi ya ziada kuondosha hatari baada ya kuchenga mabeki kadhaa wa Misri na kuvuta shuti kabla ya Kahraba kufungia timu yake bao.

Kenya pia ilinufaika na pasi mbovu ya nyuma kuadhibu Wamisri katika dakika ya 67. Beki wa zamani wa Arsenal, Mohamed Elneny, ambaye kocha El Badry alimuingiza kama mchezaji wa akiba, alipiga pasi kwa kipa wake ambayo Kenya iliiba kabla ya mshambuliaji wa Kashiwa Reysol, Olunga kukamilisha kwa ustadi.

Stars, ambayo ilikuwa imechabangwa mara tano mfululizo ikifunga bao moja na kufungwa 13 na Misri katika mechi hizo, ilistahimili mashambulizi makali dakika za mwisho.

Vijana wa Kimanzi wataalika Togo katika mechi yao ya pili itakayosakatwa Novemba 18 katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.

Togo ilianza kampeni yake vibaya pale ilipokung’utwa 1-0 jijini Lome na wanavisiwa wa Comoros. Faiz Selemani alitikisa nyavu za Togo dakika ya 51. Comoros, ambayo inaongoza kundi hili, itakuwa mwenyeji wa Misri mnamo Novemba 18.

Vikosi vya MISRI na KENYA:

Kenya

Wachezaji 11 wa kwanza – 18. Patrick Matasi (kipa), 1. Ian Otieno (kipa) ‘9), 13. Samuel Olwande, 3. Erick Ouma, 2. Joseph Stanley, 5. Joash Onyango, 12. Victor Wanyama (nahodha), 10 Eric Johana, 17. Lawrence Juma, 14. Michael Olunga, 8. Johana Omollo (15. Kenneth Muguna ‘62) 7. Ayub Timbe (16. Cliff Nyakeya ‘29). Wachezaji wa akiba – 1. Ian Otieno (kipa), 4. Haron Shakava, 22. Johnstone Omurwa, 6. Anthony Akumu, 16. Cliff Nyakeya, 15. Kenneth Muguna, 20. Whyvone Isuza, 11. Jesse Were, 9. John Makwata, 21. Bonface Muchiri, 19 Hillary Wandera, 23. Timothy Odhiambo.

Misri

Wachezaji 11 wa kwanza – 1. Mohammed Elshenawy (kipa), 3. Abdallah Gomaa, 6. Ahmed Hegazi, 7. Ahmed Fathy, 8. Tarek Hamed, 9. Hussein Elshahat (23. Ahmed Zizo ‘56) 11. Mahmoud Kahraba (22. Mohamed Afsha ‘64) 14. Amro El Solaya, 20. Mahmoud Alaa, 21. Mahmoud Treziguit. Wachezaji wa akiba – 2. Baher ElMohamady, 4. Mohammed Hany, 5. Ramy Rabia, 10. Marwan Hamdy, 12. Ayman Ashraf, 13. Mahmoud Wahid, 15. Ahmed Gomaa, 16. Mohammed Awad, 17. Mohamed ElNeny, 18. Hossam Hassan, 19. Karim Tarek, 23. Ahmed Zizo,22. Mohamed Afsha.