Michezo

Kenya yavuna medali 10 riadha za Afrika za chipukizi zikipamba moto Ivory Coast

April 19th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

FANCY Cherono alitifulia wenzake vumbi akishindia Kenya dhahabu katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji Alhamisi kwenye Riadha za Afrika za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 na 20 yanayopamba moto jijini Abidjan, Ivory Coast.

Cherono aliongoza Mkenya mwenzake Caren Jeruto kufagia nafasi mbili za kwanza katika riadha za Unde-20.

Ilikuwa siku nzuri kwa Kenya kwa sababu ilizoa jumla ya medali 10.

Wakenya wengine waliovuna medali Alhamisi ni Zena Jemutai aliyeongoza Mkenya mwenzake  Deborah Chemtai kufagia dhahabu na fedha katika mbio za mita 3000; Kibet Chepkwony (fedha) na Ronald Kipngetich (shaba) wakaridhika na medali hizo katika mbio za Under-18 za mita 2000 kuruka viunzi na maji, Brian Tinega akanyakua nishani ya fedha katika mbio za mita 400 za Under-18 nao Linda Kageha (mita 400 wasichana Under-18) na Edinah Jebitok (mita 1500 Under-20) wakaridhika na fedha.

Mercyline Cherono alijishindia medali ya shaba katika mbio za mita 1500 baada ya kumaliza nyuma ya Jebitok.