Kenya yazidi kuteleza Olimpiki za Walemavu

Kenya yazidi kuteleza Olimpiki za Walemavu

Na MASHIRIKA

MAKALA ya Olimpiki za Walemavu mwaka huu jijini Tokyo, Japan yatashuhudia Kenya ikisajili matokeo duni zaidi katika mashindano hayo chini ya kipindi cha miaka 21 iliyopita.

Hapo jana, matumaini finyu ya Kenya kuzoa nishani mbili katika mbio za 1,500m T11 wanawake yalisalia mikononi mwa Nancy Chelangat Koech pekee baada ya Mary Waithera Njoroge kubanduliwa kwenye hatua ya mchujo.

Akielekezwa na Bernard Korir, Waithera aliambulia nafasi ya tatu kwa muda bora wa dakika 4:52.54 kwenye kundi la kwanza la lililotawaliwa na Olivia Rodriguez wa Mexico (4:47.27) na Shanshan He wa China (4:52.40).

Licha ya kumaliza wa nne katika kundi la pili la mchujo, muda wa kasi (4:51.68) uliosajiliwa na Chelangat chini ya uelekezi wa kaka yake Geoffrey Kiplangat Rotich ulimkatia tiketi ya fainali iliyoandaliwa leo asubuhi katika uwanja wa kitaifa wa Tokyo.

Kundi la Chelangat lilitawaliwa na Louzanne Coetzee wa Afrika Kusini (4:49.24) na Susana Rodriguez wa Uhispania (4:51.38). Joanna Mazur wa Poland pia aliingia fainali baada ya kusajili muda wa kasi (4:51.67) uliomweka katika nafasi ya tatu mbele ya Chelangat ambaye ni mkazi wa eneo la Londiani, Kaunti ya Kericho.

Chelangat aliyezaliwa bila uwezo wa kuona, aliwahi kunogesha fani mbili kwenye Olimpiki za Walemavu mnamo 2016 jijini Rio de Janeiro, Brazil.

Aliambulia nafasi ya 16 katika mbio za 200m na akazoa nishani ya fedha katika 1,500m (4:42.14).Mnamo 2019, alishinda medali ya shaba katika 1,500m (4:56.28) kwenye Riadha za Dunia zilizoandaliwa Dubai.

Chelangat alijaajaa ugani kwa fainali kabla ya Eric Kiptoo Sang na Wilson Bii kuanza kuwania tiketi za kuingia fainali ya kesho ya mbio za 1,500m T11 – kategoria inayoshirikisha wanariadha walio na viwango tofauti vya uwezo wa kuona.

Matumaini ya Kenya kuingia fainali ya kiwango cha ‘B’ kwenye fani ya upigaji makasia pia yalizimika jana baada ya Asiya Sururu Mohammed kuambulia nafasi ya sita (dakika 14:27.48).

Awali, alikamata nafasi ya tano (13:14.26) kwenye mchujo wa pili wa kategoria ya PR1 Single Sculls kutafuta nafasi nzuri kwenye msimamo wa orodha ya dunia.

Wakenya walizoa jumla ya medali sita – dhahabu tatu, fedha moja na shaba mbili kwenye Olimpiki za Walemavu 2016 nchini Brazil.

Katika jumla ya makala 11 yaliyopita ya michezo hiyo, Kenya imejizolea jumla ya medali 48 – dhahabu 19, fedha 16 na shaba 13.Makala ya 2008 jijini Beijing, China ndiyo yaliyowapa Wakenya jukwaa maridhawa zaidi la kutamba baada ya kujishindia dhahabu tano, fedha tatu na shaba moja.

Makala ya mwaka huu ambayo yatatamatika rasmi Septemba 5 na hapo kesho kwa Team Kenya, ni ya 12 kwa taifa hili kushiriki tangu inogeshe kivumbi cha kwanza mnamo 1972 jijini Heidelberg, Ujerumani na kuzoa dhahabu ya uogeleaji (25m freestyle) kupitia John Britton.

Kenya ndio washikilizi wa rekodi za dunia kwenye Olimpiki za Walemavu katika mbio za 1,500m T11 (3:58.37, Samwel Muchai), 5000m T11 (15:11.07, Henry Wanyoike), 5000m T12 (31:42.97, Henry Kirwa) na 10,000m T11 (31:37.25, Henry Wanyoike).

You can share this post!

Ruto na Kalonzo kumenyana tena Ukambani

Taharuki yatanda mpakani watu 3 wakiuawa