Michezo

Kenya yazoa medali 46 Riadha za Afrika

April 21st, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA ilikamilisha Riadha za Afrika chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 na miaka 20 kwa jumla ya medali 46 mjini Abidjan nchini Ivory Coast mnamo Aprili 20, 2019.

Kwa mara ya kwanza kabisa katika mashindano haya, Kenya ilizoa medali katika fani ambazo imekuwa haitumi wawakilishi ama imekuwa ikifanya vibaya sana.

Baada ya siku tano za mashindano haya yaliyoanza Aprili 16, Kenya ilikuwa na medali 19 za dhahabu, 16 za fedha na 11 za shaba.

Faith Kipsang alishangaza katika kuruka umbali (Long Jump) aliponyakua nishani ya dhahabu ya Under-20 naye Denis Kangogo akazoa medali ya kuruka hatua tatu (Triple Jump).

Katika siku ya mwisho, Edward Zakayo ni mmoja wa wakimbiaji waliofanya wimbo wa taifa wa Kenya kuchezwa.

Zakayo alinyakua taji la mbio za mita 5,000 baada ya kushinda mizunguko hiyo 12 na nusu kwa dakika 13 na sekunde 13.06.

Aliongoza Wakenya wenzake Jacob Krop (13:14.44) na Reuben Poghisho (13:43.46) kufagia nafasi tatu za kwanza mtawalia.

Matokeo haya yaliridhisha kiongozi wa msafara wa timu ya Kenya, Barnabas Korir kiasi cha kusema, “Inafurahisha kuona kwamba Kenya inapata medali katika fani za uwanjani kama Triple Jump na Long Jump. Hii ni historia nzuri sana.”