Habari Mseto

Kenyatta afungua kiwanda cha saruji

January 28th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta ameongoza Jumanne hafla ya ufunguzi wa kiwanda cha kutengeneza saruji chenye thamani ya Sh5.8 eneo la Salgaa, Kaunti ya Nakuru ambacho kinatarajiwa kubadili uchumi wa eneo hilo.

Kiwanda cha Simba Cement kina uwezo wa kutoa nafasi 700 za ajira na kitastawisha sekta ya ujenzi wa nyumba kwa kuwezesha upatikanaji wa saruji kwa bei nafuu.

Kiwanda hicho ambacho kingali kinapanuliwa tayari kimewaajiri Wakenya 300 na inakisiwa kuwa kufikia mwezi Juni 2020 kitachangia kubuniwa kwa nafasi zaidi za ajira.

Akiongea na wakazi wa eneo hilo, wafanyakazi na wageni walioalikwa, Rais amezihimiza kampuni zinazohusika na sekta ya ujenzi kutumia saruji ya gharama nafuu kutoka kiwanda hicho kupanua biashara zao na akatoa hakikisho kuwa serikali inamakinika kuvutia viwanda zaidi katika eneo hilo.

Waziri wa Mafuta na Uchimbaji Madini John Munyes amesema hitaji la saruji sasa limeongezeka hapa nchini na pia katika kanda hii hasa nchini Sudan Kusini na Kusini mwa Ethiopia.

Bw Munyes amesema nchi hii ina hifadhi kubwa ya madini ya chokaa na malighafi nyinginezo zinazotumiwa kutengeneza saruji na akahimiza sekta ya kibinafsi kuwekeza zaidi katika sekta ya ujenzi wa nyumba.

Mwenyekiti wa kampuni ya Devki Narendra Raval amesema kiwanda hicho kinauza saruji kwa Sh530 kwa mfuko mmoja wa kilo 50 mjini Nakuru na viunga vyake badala ya Sh750.