Michezo

#KenyaVsGhana: Mechi ilivyoletea Kenya mamilioni

September 11th, 2018 1 min read

Na Geoffrey Anene

MASHABIKI 17, 312 pekee ndiyo walionunua tiketi kushuhudia mechi kati ya Kenya na Ghana katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani unabeba mashabiki 60, 000 iliyosakatwa Septemba 8, 2018.

Hii ni baada ya kampuni iliyosimamia masuala ya tiketi ya mchuano huo wa kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019, Big Brother Events Agency kutangaza Jumatatu kwamba Sh3, 873,600 (Dola za Marekani 38,262) ndizo zilikusanywa kutokana na mauzo ya tiketi.

Kampuni hiyo imeambia tovuti ya Futaa kwamba iliuza tiketi 514 za watu mashuhuri (VIP). Kila tiketi ya VIP ilinunuliwa kwa Sh1,000 kumaanisha kwamba tiketi hizi zilichangisha Sh514,000.

Tiketi 16, 798 za watu wa kawaida ziliuzwa. Bei ya tiketi hizi ilikuwa Sh200 kumaanisha kwamba Sh3,359,600 zilipatikana kutokana na mauzo ya tiketi za watu wa kawaida.

Katika kikao na wanahabari Septemba 7, Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa alisema Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) linaruhusu watu wasiozidi 50, 000 uwanjani humo, ingawa hakutangaza wazi kama idadi hii ya tiketi ndiyo ilichapishwa.