Michezo

#KenyaVsGhana: Nyota watakaokosa mechi

September 7th, 2018 1 min read

Na Geoffrey Anene

MANAHODHA Victor Wanyama (Kenya) na Asamoah Gyan (Ghana) ni baadhi ya majina makubwa yatakayokosa mechi muhimu kati ya Harambee Stars na Black Stars ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) uwanjani Kasarani hapo Septemba 8, 2018.

Kiungo wa Tottenham Hotspur Wanyama bado hajapona kabisa jeraha lake, ingawa kuna madai klabu hiyo ya Uingereza imemkwamilia ikihofia jeraha lake la goti litakuwa baya zaidi akihusishwa katika mchuano huu.

Kenya, ambayo inaongoza na kocha Mfaransa Sebastien Migne, itakosa huduma za kiungo mshambuliaji Ayub Timbe kutoka Beijing Renhe nchini Uchina na Brian Mandela kutoka Maritzburg United nchini Afrika Kusini wanaotumikia marufuku kutokana na kuonyeshwa kadi na Paul Were kutoka klabu ya Kaisar nchini Kazakhstan) ambaye yuko mkekani na jeraha.

Kuna hofu kuhusu mvamizi Jesse Were na beki David Owino, ambao wanasakata soka yao ya malipo Zesco United nchini Zambia. Wawili hawa wana majeraha madogo ya misuli ya paja.

Kocha Kwesi Appiah wa Ghana aliwacha nje nahodha Gyan, naibu wa nahodha Andre Ayew na Jordan Ayew, ambao wanachezea klabu za Kayserispor na Fenerbahce nchini Uturuki na Crystal Palace, mtawalia. Mabeki Kassim Nuhu kutoka klabu ya 1899 Hoffenheim nchini Ujerumani na John Boye kutoka Metz nchini Ufaransa waliumia.

Ghana inaongoza Kundi F kwa alama tatu kutokana na ushindi wake wa mabao 5-0 dhidi ya Ethiopia mwaka 2017. Kenya ni ya tatu bila alama baada ya kulemewa na Sierra Leone 2-1 jijini Freetown.