Kepa Arrizabalaga kati ya wanasoka sita wa akiba watakaotegemewa na Uhispania kwenye Euro iwapo kikosi cha kwanza kitaathiriwa zaidi na corona

Kepa Arrizabalaga kati ya wanasoka sita wa akiba watakaotegemewa na Uhispania kwenye Euro iwapo kikosi cha kwanza kitaathiriwa zaidi na corona

Na MASHIRIKA

KIPA Kepa Arrizabalaga wa Chelsea amejumuishwa katika kikosi cha akiba kitakachotegemewa na Uhispania iwapo kikosi cha kwanza kitaathiriwa na janga la corona.

Kepa aliitwa kambini mwa kikosi hicho kitakachokuwa kikishiriki mazoezi sambamba na kikosi cha kwanza siku chache baada ya kiungo na nahodha Sergio Busquets kupatikana na virusi vya corona.

Uhispania walijiondoa kwenye mchuano wa kirafiki dhidi ya Lithuania mnamo Juni 8 na badala yake wakawawajibisha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 21 kwenye gozi hilo lililowavunia ushindi wa 4-0.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF), wanasoka na wafanyakazi wote waliopatikana na virusi vya corona kwa sasa wamejitenga.

Fowadi Rodrigo Moreno wa Leeds United na kiungo Pablo Fornals wa West Ham United pia wameitwa katika kambi ya ziada ya Uhispania pamoja na Carlos Soler (Valencia), Brais Mendez (Celta Vigo) na Raul Albiol (Villarreal).

Wanasoka hao wa akiba hawatakuwa katika kambi ya mazoezi ya Uhispania ya Las Rozas wala kuchanganyika na wenzao wa kikosi cha kwanza. Wataitwa tu kuwajibikia timu iwapo maambukizi ya corona yataripotiwa katika kikosi cha kwanza.

Baada ya kufungua kampeni zao za Euro dhidi ya Uswidi mnamo Juni 14, Uhispania watavaana na Poland mnamo Juni 19 kisha Slovakia siku nne baadaye. Uhispania wanaazimia kuwa kikosi kinachojivunia mafanikio makubwa zaidi kwenye kipute cha Euro.

Kwa upande wao, Uswidi watapania kuwa na mwanzo bora utakaoweka hai matumaini yao ya kusonga mbele zaidi ya hatua ya makundi ya Euro kwa mara ya kwanza tangu 2004 ambapo walitinga robo-fainali. Kikosi hicho kiliondolewa kwenye hatua ya nusu-fainali mnamo 1992.

Ushindi uliosajiliwa na makinda wa Uhispania dhidi ya Lithuania kirafiki uliendeleza rekodi nzuri ya kutoshindwa kwa miamba hao katika jumla ya mechi nane mfululizo huku wakishinda mechi tatu kati ya nne zilizopita.

Sawa na Ujerumani waliotawazwa mabingwa wa dunia mnamo 2014, Uhispania walioibuka wafalme wa dunia mnamo 2010, walitia kapuni taji la Euro mnamo 1964, 2008 na 2012.

Kampeni za Euro mwaka huu ni jukwaa zuri kwa Uhispania kurejesha ubabe wao katika ulingo wa soka baada ya kubanduliwa mapema katika hatua ya makundi kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2014 nchini Brazil. Kikosi hicho pia kilidenguliwa katika hatua ya 16-bora kwenye Euro 2016 na Kombe la Dunia 2018 nchini Ufaransa na Urusi mtawalia.

“Uhispania ni miongoni mwa timu bora duniani. Lakini tuna kikosi imara kilicho na uwezo wa kutatiza miamba hao kwa dakika 90,” akasema kocha wa Uswidi, Janne Andersson atakayetegemea zaidi wavamizi Marcus Berg na Alexander Isak katika mfumo wa 4-4-2.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Zesco United yanyanyua taji la Ligi Kuu Zambia

BB Erzurumspor yatema Johanna Omolo baada ya kushushwa...