Habari Mseto

Kericho, Bomet kufikishwa kortini kwa kuhudumu bila mwakilishi mlemavu

December 21st, 2018 1 min read

Na Anita Chepkoech

MAWAKILI kutoka Bonde la Ufa Kusini sasa wanapanga kupinga uhalali wa kisheria wa kaunti za Kericho na Bomet ambazo hazina wawakilishi wa watu wanaoishi na ulemavu kwenye mabunge yao jinsi inavyotakikana kisheria.

Mwenyekiti wa Chama cha Kisheria(LSK) tawi la Bonde la Ufa kusini Geofrey Kipng’etich alisema kwamba wanapanga kuvihoji vyama vya kisiasa ili kupata sababu zao za kutoteua hata mwakilishi moja mlemavu katika mabunge ya kaunti hizo mbili.

Akizungumza katika Shule ya Msingi ya Tonongoi wakati wa sherehe za mapema za krismasi kwa watoto walemavu 50 Bw Kipng’etich alisema kwamba japo kaunti ya Bomet ina mwakilishi moja mteule mlemavu, kaunti jirani ya Kericho haina mwakilishi mlemavu kabisa.

“Tutalazimika kuwasilisha hoja mahakamani kujua uhalali wa mabunge hayo. Tunahitaji kujua sababu za walemavu kupigwa teke kwenye mchakato mzima wa uteuzi ilhali kuna maswala muhimu ambayo hayawezi kutekelezwa bila uwepo wao bungeni,” akasema Bw Kipng’etich.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Hakimu Mkuu wa mahakama ya Kericho Mumbi Ngugi, Hakimu Mkuu Mkaazi wa mahakama hiyo Samuel Mokua, hakimu Solomon Ng’etich na mwakilishi kutoka ofisi ya DPP.

Wakuu hao waliwapa watoto hao vyakula, malazi na vifaa muhimu vya masomo kwa wanafunzi walemavu.