Habari

KERO LA NAULI: Wakenya waanza kuumia

September 3rd, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

TAYARI Wakenya wameanza kuhisi joto la kupandishwa kwa ushuru wa asilimia 16 ya VAT kwenye bei ya mafuta, baada ya wahudumu wa usafiri kupandisha nauli na kuwalazimisha abiria kulipa zaidi.

Wahudumu wengi Jijini Nairobi walipandisha nauli kuanzia Jumatatu, mengi ya maeneo yakishuhudia kupanda kwa kati ya Sh10 na Sh20 kulingana na wakati wa siku.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kuwa wengi wa wahudumu kwenye sekta ya usafiri wameongeza nauli, ili kugharamia kupanda kwa bei ya mafuta, mzigo wote ukimwangukia Mkenya wa kawaida, ambaye bila jingine la kufanya aliishia kutii amri.

Wahudumu waliozungumza na Taifa Leo walisema walilazimika kumpokeza Mkenya mzigo wa gharama, baada ya bei a mafuta kupanda vikubwa na hivyo kuongeza kiwango cha matumizi ya mafuta.

“Kama hapa huwa tunalipisha Sh30 wakati wateja ni wachache na Sh60 asubuhi na jioni (rush hour), lakini sasa tumepandisha nauli hiyo kwa Sh10. Gari lilikuwa likitumia mafuta ya Sh5,000 kwa siku lakini sasa litatumia Sh6,500,” akasema mhudumu wa gari la kwenda Wangige.

Maeneo yaliyoadhirika jijini ni pamoja na Thika, Juja, Kahawa West, Kasarani, Uthiru, Banana, Kangemi, Limuru na Juja.

Katika steji ya Mololine kwenda Nakuru, Eldoret na Kisumu, hali ilikuwa sawia, japo kiwango kilichopandishwa kikiwa kikubwa. Wasafiri wa kuelekea Nakuru, Eldoret na Kisumu wakipandishiwa nauli hadi 500, 1000, 1,200 kutoka Sh300, Sh800 na Sh1000 mtawalia.

Wahudumu walisema wateja wengi hawakupokea vyema ujumbe wa kupanda kwa nauli, wakisema wengine walisusia huduma.

Lakini kwa jumla nauli zilipanda kwa kati ya Sh50 na Sh300 kwa wasafiri wa nyendo ndefu, japo wahudumu wengine wakikosa kuongeza nauli.

Wale ambao hawakupandisha walisema walinuia kufanya hivyo baada ya kuanza kutumia mafuta yaliyolipizwa ushuru huo.