Habari Mseto

Kero mtoto kubakwa kisha kukatwa sehemu nyeti kwa wembe

January 9th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

FAMILIA moja kutoka kaunti ya Homa Bay inalilia haki kutoka kwa serikali, baada ya mtoto wao wa miaka 13 kunajisiwa na wakora kisha kukatwa sehemu zake za siri kwa wembe na kijiti walipomaliza unyama wao.

Inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo wa darasa la nane alikuwa ametoka nje kwenda haja usiku wa Alhamisi wiki iliyopita, wakati mara moja alinyongwa shingoni na kuvutwa mguuni hadi karibu na lango la nyumbani kwao.

“Mtu akanishika shingo, sikuweza kupata sauti ya kupiga nduru. Mtu akanishika mguu akanipeleka karibu na geti,” akasema mtoto huyo, akiwa hospitalini ambapo anapokea matibabu.

Mzazi wake alisema kuwa wanaume hao, ambao bado hawajajulikana walimtendea unyama hadi akazirai.

Wakaribu kumnajisi wakapata sehemu yenyewe ni ndogo, wakachukua wembe na kumkata sehemu ya siri hadi kwenye shimo la choo. Ndio wakaanza kumnajisi,” akasema mama huyo, akiwa na uchungu.

“Kisha walipomaliza wakachukua kijiti na kukoroga ndani.”

Tukio hilo liliwacha wanakijiji kwa hofu, huku wakitoa kilio kwa polisi kuharakisha uchunguzi na kukamata washukiwa wa unyama huo.

Mtoto huyo naye anatarajia kufanyiwa upasuaji ili kurekebisha sehemu za siri ambazo ziliharibika.

“Tunaomba usaidizi, mtoto huyu anapitia uchungu sana kwani wenzake wakisoma naye hawezi enda shule. Si sawa kwa binadamu,” akasema mama mmoja jirani yake.

Familia ya mtoto huyo sasa inawataka polisi kuhakikisha kuwa waliomfanyia mtoto wao hivyo wanakamatwa.