Habari Mseto

Kero ya majitaka Githurai kutatuliwa

October 16th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

SUALA la majitaka katika mtaa wa Githurai 45 ulioko eneobunge la Ruiru limekuwa kero kwa miaka mingi, barabara zikikosa kupitika hususan msimu wa mvua.

Wafanyabiashara wanaosukuma gurudumu la maisha kandokando mwa barabara, hasa barabara inayounganisha mtaa huo na Progressive, Mumbi na Mwihoko, hulazimika kufunga maduka kwa sababu ya kuhangaishwa na majitaka.

Huenda matatizo hayo hivi karibuni yakafikia kikomo kupitia mradi wa ukarabati wa mitaro ya majitaka unaoendelea.

Septemba 6, 2019, mbunge wa Ruiru Simon King’ara alizindua ukarabati wa mitaro ya majitaka na barabara eneo hilo. “Hatua hii inalenga kuimarisha miundomsingi,” akasema mbunge huyo.

Shughuli hiyo inayofadhiliwa na serikali ya kitaifa inaendelea. Ili kutatua kero ya majitaka yanayofuja msimu wa mvua, ukarabati ulianzia eneo la Reli na umefikia katika duka la kijumla la Kassmatt Jumbo.

“Maji haswa yale taka hutuhangaisha sana. Mvua inapozidi barabara hazipitiki. Ujenzi unaoendelea ni afueni kwetu,” James Njoroge, mfanyabiashara amesema.

Hata hivyo, inasemekana kiini cha maji yanayosambaa barabara inayounganisha Githurai na Mwihoko ni yatokayo Thika Super Highway.

Mhudumu mmoja wa tuktuk ameeleza Taifa Leo kuwa endapo chanzo chake hakitaangaziwa huenda ukarabati huo ukakosa kuzaa matunda. “Nina ramani ya chochote kinachojiri katika barabara hii. Mwanakandarasi asipoweka mikakati ya kuteka maji yanayotoka Thika Super Highway msimu wa mvua, hali itakuwa mbaya zaidi,” akaonya.

Baadhi ya maeneo ya barabara hiyo kuu inayounganisha Thika na jiji kuu la Nairobi yamekuwa yakishuhudia mafuriko.

Mbunge wa Ruiru Simon King’ara pia amehimizwa kuingia katika vitongoji vya mtaa wa Githurai ili kuangazia kero ya majitaka. Kabla ya ujenzi, halmashauri ya kitaifa ya ujenzi – NCA huagiza wamiliki wa majumba kuhakikisha wamezingatia suala la majitaka.

Halmashauri ya kitaifa ya mazingira, Nema, inajukumika kuhakikisha mazingira ni safi na salama kwa wakazi. Maeneo mengi kaunti ya Nairobi na Kiambu, mifereji ya maji imepitishwa kwenye mitaro ya majitaka, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya watumizi wa maji hayo.