Kero ya umeme kukatika kila mara Kang’oo

Kero ya umeme kukatika kila mara Kang’oo

Na LAWRENCE ONGARO

WAHUDUMU wa bodaboda katika kijiji cha Kang’oo, Gatundu Kaskazini wamelalamika kwamba kazi yao inaharibiwa na hali ya umeme kupotea kila mara.

Mhudumu wa bodaboda katika kijiji hicho Bw John Karumu anasema kuwa ifikapo saa mbili za usiku wakazi wa kijiji hicho hukosa umeme kwa sababu unapotea ghafla.

“Kuna transfoma ambayo ndiyo hulipuka kila mara na kutuharibia biashara yetu. Hata kituo cha biashara katika kijiji hiki pia hukumbwa na hali hii,” alisema Bw Karumu.

Wakazi hao wanaitaka kampuni ya Kenya Power kufanya hima kuona ya kwamba transfoma hiyo inarekebishwa mara moja.

Alieleza kuwa wahudumu wa bodaboda hulazimika kufunga kazi mapema kuliko kawaida, kumaanisha kwamba ni hali inayorudisha chini shughuli zao za kujitafutia riziki.

Wakazi hao wametoa wito kwa viongozi wa eneo hilo kujitokeza kuona ya kwamba wanaendesha shughuli zao kama kawaida.

Bw Karumu alieleza kuwa kukosekana kwa umeme ni changamoto kubwa kwa wakazi wa kijiji hicho kwa sababu kuna visa vya utovu wa nidhamu huku uhalifu ukikithiri.

Alieleza kuwa ifikapo saa kumi na mbili za jioni kila mmoja hulazimika kuwa nyumbani ili asikutane na wahalifu wanaohangaisha wakazi wa kijiji hicho.

Naye mhudumu mwingine wa bodaboda, Bw Peter Mwaura, anasema biashara yao imezorota sana kwa zaidi ya miezi miwili sasa.

“Hali ya maisha imekuwa ngumu kwetu kwa sababu shida zetu hazijatatuliwa jinsi inavyostahili. Sisi tungetaka hali hiyo itatuliwe mara moja ili nasi tuendelee na shughuli zetu za kawaida,” alisema Bw Mwaura.

Alisema kutoka mwendo wa saa moja za usiku wakazi wa kijiji hicho huwa tayari wamerejea kwenye makazi yao huku wakihofia usalama wao kutokana na giza inayoshuhudiwa kila mara.

“Kwa hivyo, serikali ifanye jambo kuona ya kwamba watu wanaendelea na shughuli zao kama hapo awali,” alisema Bw Mwaura.

Wakazi hao wanatoa wito kwa viongozi wa eneo hilo kuchukua jukumu kuona ya kwamba shida hiyo inarekebishwa haraka iwezekanavyo.

You can share this post!

Pigo kwa Spurs baada ya mshambuliaji Son Heung-min kupata...

ODONGO: Kitui, Kibwana, Muturi na Karua wana mtihani