Michezo

Kerr achemka kusikia Innocent Wafula anapania kumtoroka

August 15th, 2018 1 min read

NA CECIL ODONGO

KOCHA  wa Gor Mahia Dylan Kerr haonekani kupumzika wala kupumua kutokana na wachezaji wake kuandamwa na klabu mahiri barani na Afrika Mashariki.

Saa chache tu baada ya kukemea majagina wa soka ya Afrika Kaizer Chiefs kwa kumsaini beki Godfrey Walusimbi bila kufuata sheria, Kerr sasa kageukia mibabe wa soka nchini Uganda,  Vispers SC baada ya taarifa kuibuka kwamba wanalenga kumnyakua beki mwengine Innocent Wafula.

“Sijasikia kwamba ofa yoyote imewasilishwa klabuni na Vispers SC ikilenga kutwaa huduma za Innocent Wafula. Iwapo wanalenga kumsaini na wameongea naye binafsi bila kuhusisha klabu basi hawajafuata sheria na sitambui usajili kama huo. Kulingana  nami hakuna chochote rasmi katika habari hizo,” akadai Kerr.

Aliongeza kwamba Wafula ni mchezaji wa Gor Mahia kulingana na mkataba aliousaini na haendi popote hadi  Januari 2019 wakati mkataba huo utakapotamatika.

“Wafula ni mchezaji wetu na ana mkataba nasi. Ni mhimili mkubwa kikosini na tegemeo letu, haendi popote,” akahitimisha Kerr.