Michezo

Kerr sasa halali akifikiri jinsi leseni ya ajenti wa Walusimbi itafutwa

August 15th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Mabingwa mara 16 wa KPL Gor Mahia, Dylan Kerr ameapa kwamba atahakikisha leseni ya ajenti wa mlinzi Godfrey Walusimbi imefutiliwa mbali.

Kerr kwa mara ya kwanza amejitokeza na kutoa kauli yake kuhusu uhamisho wa Walusimbi kutoka Gor Mahia hadi kwa  mibabe wa soka ya Afrika Kusini Kaizer Chiefs.

Kulingana na kocha huyo, Walusimbi, ajenti wake na Kaizer Chiefs wanafaa kuadhibiwa vikali kwa kukiuka sheria za uhamisho wa wachezaji kulingana na Shirikisho la soka duniani, FIFA.

“Mwenyekiti wangu, Afisa Mkuu Mtendaji wa klabu au mimi hawapaswi kulaumiwa kwa sababu uhamisho wa Walusimbi ulichangiwa pakubwa na ajenti mkorofi ambaye mimi binafsi nitahakikisha ameadhibiwa vikali,” akawaka Kerr wakati wa mahojiano.

Aidha mkufunzi huyo alilamika kwamba hiyo si mara ya kwanza kwa wawili hao kuvuruga matayarisho ya timu yake  kwa kuwa hali kama hiyo ilichangia Gor kupoteza mechi dhidi ya Esperance mapema mwaka huu(Februari, 2108).

“Wameangusha usimamizi wote wa timu hii. Waliwahi kufanya vivyo hivyo kabla ya mechi tuliyoishia kupoteza dhidi ya Esperance mwezi Februari ambayo hakushiriki kutokana na kitendo sawa na hiki,” akawaka Kerr.

Ingawa hivyo, alisisitiza kwamba hatua ya mashabiki kutaka kujua kwa nini klabu imemwaachilia mwanasoka huyo  haifai kushtumiwa kwa kuwa ni haki yao kufahamu aliko kila mchezaji wa timu wanayoshabikia.

“Ajenti wa Walusimbi ni mtu aliyejawa na tamaa na ulafi mkubwa na Kaizer Chiefs wanafikiria kwamba watampata wakitumia hela zao kwa kukiuka sheria za CAF na FIFA.

Kifungu cha sheria nambari 18 inasema kwamba klabu inayohitaji huduma za mchezaji wa klabu nyingine lazima ajulishe klabu mwenyeji kwa maandishi kabla ya kushauriana na mchezaji mwenyewe.

Walusimbi ana kandarasi na Gor hadi 2020 wala Kaizer Chiefs bado hawajatuandikia kuonyesha nia ya kumsajili,” akafafanua Kerr