Habari

Kesi dhidi ya bodi ya Mama Ngina Waterfront yatupwa

November 23rd, 2019 1 min read

Na PHILIP MUYANGA

BODI ya usimamizi iliyokuwa imeteuliwa na Waziri wa Utalii kusimamia eneo la kujipumzisha la Mama Ngina Waterfront lililokarabatiwa kwa Sh460 milioni inaweza kuendelea na kazi yake baada ya kesi iliyopinga kuwepo kwake kutupiliwa mbali.

Jaji Eric Ogola alitupilia mbali kesi hiyo iliyowasilishwa na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu na wakazi watano wa Mombasa.

Hii ni baada yao kukosa kufika mahakamani wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo.

“Ombi lililowasilishwa mnamo Novemba 8 linatupiliwa mbali bila maagizo yoyote ya gharama ya kesi,” alisema Jaji Ogola.

Kesi hiyo ilikuwa imewekwa mahakamani na kundi la kutetea haki za kibinadamu la Haki Africa, Institute for Land Governance and Human Rights na wakazi hao watano.

Walikuwa wadai kuwa iwapo bodi hiyo itakubaliwa kusimamia eneo hilo la Mama Ngina Waterfront, wachuuzi wa Mombasa watakuwa hawana mahali pa kufanyia biashara jambo ambalo litafanya washindwe kulea familia zao.

“Wachuuzi wa humu Mombasa ambao wanafanya biashara zao katika eno hili wanaweza kuzuiliwa na leseni zinaweza kutolewa kwa watu ambao sio wakazi wa Mombasa, kampuni au watu ambao wana uwezo wa kuzilipia,” wenye kesi hao walisema.

Walikuwa pia wameelezea wasiwasi wao wa kuwa Mama Ngina Waterfront ingeweza kufanywa eneo la watalii tu wa kigeni na kuwazuia wakazi kutopata nafasi ya kufika huko kujifurahisha.

Mashirika hayo ya haki za kibinadamu yalikuwa yanataka ilani ya gazeti rasmi la serikali lililokuwa na taarifa ya kuwateua wakurugenzi hao ifutiliwe mbali.

Walikuwa wanataka pia agizo la kuzuia bodi hiyo kutotwaa majukumu ya usimamizi wa eneo hilo kutoka kwa serikali ya kaunti ya Mombasa.

Wanasema kuwa sehemu hiyo ya Mama Ngina Waterfront ni eneo la umma chini ya kifungu 62(1) (a) na au (b) cha katiba ya Kenya.