Michezo

Kesi ya Diego Costa kutolipa ushuru kuamuliwa leo

June 4th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

UAMUZI wa kesi ya kutolipa ushuru inayomhusu fowadi matata wa Atletico Madrid, Diego Costa, sasa utatolewa Juni 4, 2020.

Kwa mujibu wa mahakama inayoshughulikia keshi hiyo nchini Uhispania, Costa, 31, alishtakiwa mwishoni mwa mwaka jana kwa kosa la kulaghai taifa lake zaidi ya Sh114 milioni baada ya kukosa kulipa sehemu ya kodi ya Sh587 milioni kutokana na ada iliyotumiwa na Chelsea kumsajili kutoka Atletico mnamo 2014.

Isitoshe, sogora huyo wa zamani wa Real Valladolid, hakulipa ushuru wa jumla ya Sh112 milioni kwa minajili ya haki ya matumizi ya picha zake katika matangazo mbalimbali ya Ligi Kuu za Uingereza (EPL) na Uhispania (La Liga) kati ya 2014 na 2017.

Viongozi wa mashtaka jijini Madrid wanamkata mfumaji huyo wa timu ya taifa ya Uhispania kutumikia kifungo cha miezi sita gerezani na pia kutozwa faini ya takriban Sh64 milioni kwa makosa hayo ya kukwepa kulipa kodi.

Sheria za Uhispania zinaruhusu hukumu za vifungo visivyozidi vipindi vya miaka miwili gerezani kubadilishwa na tukio la mshtakiwa kutozwa faini.

Kwa hivyo, Costa huenda akahepa kufungwa jela iwapo atakuwa radhi kulipa faini ya Sh4.7 milioni za ziada ili asalie huru. Nyota huyo mzawa wa Brazil alijiunga upya na Atletico mnamo 2017 baada ya uhusiano wake na aliyekuwa kocha wa Chelsea, Antonio Conte, kuvurugika. Amewahi pia kuvalia jezi za Braga, Celta na Albacete nchini Uhispania.