Habari Mseto

Kesi ya Jack & Jill iliyokaa kortini kwa miaka 25 kutupwa

April 19th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu Jumatano ilitisha kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa na duka la Jack& Jill (JJ) miaka 25 iliyopita ikiwa wakurugenzi wake hawatafika kortini kutoa ushahidi ipasavyo.

Jaji Fred Ochieng alisema hatasita kutupa kesi hiyo kwa vile mlalamishi hajatosheleza matakwa ya kuwasilisha ushahidi katika kesi hiyo iliyowasilishwa kortini mwaka wa 1993.

Katika kesi hiyo  JJ imeishtaki kampuni ya kutengeneza magari ya Marshall East Africa kwa kuizia magari ambayo yaliharibika hata kabla ya kusafiri kilomita 40,000 yakisafirisha mizigo.

Mahakama ilisema kwamba haitaendelea kutoa maagizo ya muda katika kesi ambayo imekuwa kortini tangu 1993.

JJ ilipeleka magari mawili iliyokuwa imenunua kutoka kwa Marshall East Africa katika karakana yake yatengenezwe lakini kufika sasa bado kutengenezwa.

JJ inaomba kampuni hiyo ya magari iilipe magari mengine kwa vile ilikiuka mkataba wa mauzo.

Kesi hiyo itasikizwa mnamo Mei 24, 2018.