Kesi ya Jumwa kuanza mwaka 2022

Kesi ya Jumwa kuanza mwaka 2022

Na BRIAN OCHARO

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa huenda atalazimika kujitetea kortini wakati kampeni za kurithi kiti cha Gavana wa Kilifi, Amason Kingi zitakapokuwa zikiendelea.

Kesi hiyo kuhusu madai ya kuhusika katika mauaji ilikuwa imepangwa kusikilizwa kwa siku tatu mfululizo mwezi huu lakini hilo halikuwezekana.

Hii ni baada ya Bi Jumwa kuagiza mawakili wake wasimwakilishe mshtakiwa mwenzake, Bw Geoffrey Otieno Okuto.

Bw Okuto alikuwa msaidizi wa Bi Jumwa wakati kisa cha mauaji ya Jola Ngumbao kilipotokea mwaka wa 2019.

Sasa atawakilishwa na Bi Grace Okumu ambaye angali anahitaji muda kujifahamisha na kesi hiyo ambayo imepangiwa kuanza kusikilizwa Januari 2022.

Hapo awali, mawakili Jared Magolo, Cliff Ombeta, Danstan Omari na Shadrack Wamboi walikuwa wakiwawakilisha wawili hao.

Hii ni mara ya pili kesi hiyo kuahirishwa kwa sababu ya matatizo ya kutokuwa na wakili.

Wiki iliyopita, Jaji Anne Ong’injo alilazimika kuahirisha kesi hiyo baada ya Bi Jumwa kuwaondoa mawakili wote wanne ambao wamekuwa wakiwawakilisha katika kesi hiyo.

Bw Okuto pia anahitajika kutafuta mdhamini mpya baada ya kubainika kuwa kuna mipango ya kuondoa mdhamini wake.

Upande wa mashtaka umepanga kuwaita mashahidi 32 kuthibitisha kesi yake dhidi ya wawili hao.

Bi Jumwa na Okuto walikanusha mashtaka kuwa mnamo Oktoba 15 2019, walimuua Ngumbao, ambaye ni mjomba wa diwani wa Ganda Bw Reuben Katana.

Aliuawa kwa kupigwa risasi wakati Bi Jumwa, Bw Okuto na wafuasi wao walipodaiwa kuvamia nyumba ya Bw Katana na kusababisha fujo.

You can share this post!

Mawakili wamrai Kangogo ajisalimishe

Mbegu zilizotolewa kwa Sharon si za Obado, washukiwa