Kesi ya Jumwa yaahirishwa wakili Ombeta amalize kesi ya mauaji

Kesi ya Jumwa yaahirishwa wakili Ombeta amalize kesi ya mauaji

Na MWANDISHI WETU

MAHAKAMA KUU imeagiza kesi ya ufisadi inayomkabili mbunge wa Malindi, Aisha Jumwa, iahirishwe hadi kesi nyingine ambayo mmoja wa mawakili wake anashiriki Nairobi ikamilike na kuamuliwa.

Jaji Jessie Lessit aliagiza Hakimu Mkuu wa Mombasa, Edna Nyaloti kuahirisha kesi ya Bi Jumwa kwa kuwa wakili Cliff Ombeta anashiriki kesi ya mauaji ya wakili Willie Kimani ambayo Jaji Mkuu Martha Koome ameagiza iharakishwe ili ikamilike kabla ya mwezi huu.

Bi Jumwa ameshtakiwa pamoja na watu wengine sita kwa kughushi, kuhusika katika ulanguzi wa pesa na ulaghai wa Sh19 milioni za Hazina ya eneobunge lake la Malindi.

Jaji Lessit alisema kesi hiyo inafaa kuahirishwa hadi mwisho wa mwezi kwa kuwa Bw Ombetta anatetea washtakiwa katika kesi ya mauaji ya Willie Kimani.

Agizo la jaji huyo lilijiri baada ya Bi Nyaloti kulaumu Bw Ombeta kwa kuchelewesha kesi ya Bi Jumwa akijua kwamba alikuwa katika kesi ya mauaji ya wakili Willie Kimani.

Katika agizo hilo, Jaji Lessit anasema kwamba kesi ya mauaji ya wakili huyo anayosikiliza inafaa kupewa kipaumbele kuliko ya Bi Jumwa iliyo mbele ya Bi Nyaloti.

You can share this post!

Mlima wateleza kwa Ruto, Raila

Vilio vya Muturi, Waiguru vyazua maswali mengi