Habari Mseto

Kesi ya Karua dhidi ya Gavana Kamotho yagonga mwamba

August 6th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

JUHUDI za kiongozi wa chama cha Narc-Kenya Bi Martha Karua za kumng’oa mamlakani Gavana wa Kirinyaga Anne Mumbi Kamotho ziligonga mwamba Jumanne Mahakama ya Juu ilipotupilia mbali rufaa aliyokuwa amewasilisha mwaniaji huyo wa zamani wa kiti cha urais.

Kutupwa kwa rufaa hiyo kulikuwa pigo kubwa kwa Bi Karua kwa vile kulizamisha ndoto yake kuwa Gavana wa Kirinyaga.

Bi Karua amepoteza mara tatu kesi ya kumtimua mamlakani Bi Kamotho aliyefunga ndoa ya kitamaduni mnamo Julai 13 na wakili Kamotho Waiganjo katika shule moja ya msingi Kirinyaga.

Mahakama ya juu ilisema katika uamuzi uliosomwa na Jaji Isaac Lenaola kwamba kesi ya Bi Karua ilikuwa imepitwa na wakati na haingelisikizwa. Walisema rufaa ilicheleweshwa kwa muda wa siku 60

Jaji Mkuu David Maraga na majaji Mohammed Ibrahim, Jackton Ojwang, Smokin Wanjala , Njoki Ndung’u na Lenaola walisema sheria iwazi kwamba kesi inayocheleweshwa kushtakiwa itupiliwe mbali.

“Rufaa ya Bi Karua iliwasilishwa mahakamani baada ya muda wa siku 60 uliowekwa kisheria kumalizika.Hivyo basi rufaa hii imepitwa,” walisema majaji hao wa mahakama ya upeo.

Waliitupilia mbali rufaa hiyo na kutangaza kwamba Bi Waiguru ndiye mshindi halisi wa kiti cha Ugavana wa Kirinyaga.

Baada ya kufikia uamuzi Bi Kamotho alikishinda kiti hicho kwa mujibu wa sheria mahakama iliamuru tume huru ya uchaguzi na mipaka imkabidhi cheti cha ushindi mshtakiwa.

Bi Kamotho alikishinda kiti cha Ugavana wa Kirinyaga kwa kuzoa kura 153,353 naye Bi Karua akajinyakulia kura116,626.

Aliyekuwa Gavana Bw Joseph Ndathi aliweza kuzoa kura 4,496.

Katika malalamishi yake Bi Karua alisema hakupewa fursa ya kuwasilisha ushahidi kuthibitisha kwamba kura zilipigwa vibaya katika vituo 100.

Kesi ya Bi Karua ilitupiliwa mbali na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa.

Baada ya kutupwa kwa kesi hiyo ya Mahakama kuu Kerugoya majaji watatu wa mahakama ya rufaa Jaji Mohammed Warsame, Jaji Daniel Musinga na Jaji William Ouko waliamuru kesi hiyo isikizwe upya wakisema “ Bi Karua hakutendewa haki.”

Hata hivyo kesi hiyo ilitupiliwa mbali tena na akakata rufaa mjini Nyeri kisha ikatupwa.

Bi Karua mwenye bidii ya mchwa aliwasilisha tena kesi hiyo katia mahakama ya upeo akitazamia kumng’oa mamlakani Bi Waiguru.

Hata hivyo ndoto yake Bi Karua iliambulia patupu rufaa hiyo kutupwa. Sasa atasubiri uchaguzi mkuu wa 2022 kujaribu bahati yake tena.