Habari Mseto

Kesi ya kupinga noti mpya yapelekwa kwa Maraga

June 5th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KESI ya kupinga kuzinduliwa kwa noti mpya iliyowasilishwa na mwanaharakati Okiya Omtatah imepelekwa kwa Jaji Mkuu (CJ) David Maraga kuteua jopo la majaji watatu kuamua masuala mazito ya kisheria kuhusu suala hilo.

Mbali na Omtatah aliyekuwa Mbunge wa Kamkunji na ambaye sasa ni Mbunge anayewakilisha Kenya katika Bunge la Jumuia ya Afrika Mashariki (EALA) Bw Simon Mbugua pia aliwasilisha kesi sawa na hiyo akiomba uzinduzi, usambazaji na utumizi wa noti mpya uzimwe.

Wawili hawa wanaomba mahakama kuu isitishe utengenezaji na usambazaji wa noti mpya zikiwa na sura ya aliyekuwa Rais wa kwanza nchini Kenya hayati Mzee Jomo Kenyatta.

Kesi hizo ziliwasilishwa mbele ya Jaji Weldon Korir aliyeziratibisha kuwa za dharura na kuwaamuru mawakili wafike mbele ya Jaji Maraga atakayeteua jopo la majaji watatu kuamua ikiwa haki za wakenya kushirikishwa katika suala hilo la kuzinduliwa kwa noti mpya zilikandamizwa.

Akiamuru kesi hizo ziwasilishwe kwa Jaji Maraga , Jaji Korir alisema “ kuna masuala mazito ya kisheria yanayopasa kusikizwa na kutatuliwa na jaji zaidi ya mmoja.”

Bw Omtatah alikuwa wa pili kuwasilisha kesi hiyo kupinga matumizi ya noti mpya zilizozinduliwa Juni 1, 2019 na Rais Uhuru Kenyatta.

Rais Kenyatta alizindua pesa hizo wakati wa kusherehekea siku kuu ya Madaraka iliyofanyika katika kaunti ya Narok.

“Ni uwongo mtupu kwamba uzinduzi na matumizi ya noti mpya ulichapishwa katika toleo la Gazeti rasmi la Serikali la Mei 31 2019 kwa vile hakuna gazeti kama hilo lililochapishwa na Serikali,” asema Bw Omtata katika kesi aliyoshtaki Jumatatu.

Anaongeza kusema, “Hakuna habari zilizochapishwa katika toleo la Mei 31 2019 la Gazeti la Serikali kuhusu uzinduzi wa sarafu (noti) mpya za Sh50, Sh100, Sh200 ,Sh500 na Sh1000.”

Bw Omtatah pia anapinga kuwako kwa picha ya Mzee Kenyatta katika noti hizo mpya akisema inakiuka katiba.

Pia anasema marufuku ya umiliki wa noti za zamani za Sh1,000 baada ya Oktoba 1, 2019 hayaungwi mkono na sheria.

Walalamishi hawa wawili wanadai agizo noti zote za Sh1,000 zirudishwe kwa mabenki kinakinzana na haki za kikatiba na pia ni kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa Bw Omtatah amesema unzinduzi wa noti mpya ni kinyume cha kipengee nambari 231 (4) cha katiba kinachoashiria wananchi washirikishwe kabla ya maamuzi muhimu yatakayowaathiri yanapopitishwa.