Habari MsetoSiasa

Kesi ya kupinga ‘Punguza Mizigo’ kuharakishwa

July 28th, 2019 2 min read

SAM KIPLAGAT na LEONARD ONYANGO

MAHAKAMA Kuu itasikiliza kwa dharura ombi la kutaka mabunge ya kaunti yasimamishwe kujadili mswada wa mabadiliko ya katiba wa chama cha Third Way Alliance wa ‘Punguza Mizigo’.

Hii ni baada ya shirika la kisheria International Economic Law Centre (IELC) na Bw David Kamau Ngari kuibua malalamishi mbalimbali kuhusu mswada huo.

Jaji Jacqueline Kamau alielekeza Bw Ngari na shirika hilo kuweka tangazo katika magazeti, kufahamisha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), maspika wa Bunge la Taifa na Seneti na maspika wa mabunge 47 ya kaunti, kuhusu amri hiyo.

Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa kesho, ambapo Bw Ngari anahoji kuwa Third Way Alliance ilitumia hila kukusanya saini za kuunga mkono mswada huo, akisema si saini za kweli.

Bw Ngari anahoji kuwa kufanana kukubwa kwa saini kunaibua maswali kuhusu uhalali na uaminifu wa fomu ambazo IEBC ilikagua na kuidhinisha.

Anasema kuwa tume ya IEBC haikuwa na uwezo wa kukagua saini hizo, kwa kuwa haina sampuli ya saini za kufanya ulinganishaji nazo.

Vilevile, Bw Ngari alieleza korti kuwa shughuli ya ukaguzi wa saini ilifanywa kwa mikono, ilhali kisheria wapiga kura wanafaa kusajiliwa kidijitali.

Kutokana na hayo, Bw Ngari anasema ukaguzi na uidhinishaji wa saini za mswada huo ulikiuka sheria, na hivyo haufai.

Aidha, katika kesi hiyo hatua ya IEBC kuendesha shughuli ikiwa na makamishna wawili na mwenyekiti pekee imekosolewa, baada ya makamishna wanne kujiuzulu.

Bw Ngari alisema kuwa idadi ya makamishna ambao wanaruhusiwa kupokea, kukagua na kuidhinisha saini za mswada kulingana na katiba inafaa kuwa angalau watano.

“Jinsi ilivyo kwa sasa, IEBC haina ujuzi na ubora unaohitajika kikatiba kupokea na kuidhinisha mswada, nakala na saini za wapigakura jinsi zilivyopelekwa,” sehemu ya kesi hiyo inasema.

Wanataka korti isimamishe Third Way Alliance kuwasilisha mswada huo kwa mabunge 47 ya kaunti, ili ujadiliwe na kupitishwa.

Hayo yamejiri huku hisia mseto zikizidi kutolewa kuhusu mswada wa Punguza Mizigo.

Jana, Chama cha Wiper kinachoongozwa na Bw Kalonzo Musyoka kilipinga mswada huo, siku moja baada ya Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga kuelezea pingamizi zake.

Bw Musyoka alisema mapendekezo ya mswada huo hayakujumuisha maoni ya wananchi na kuongeza kwamba ukipitishwa, utaumiza wanawake na vijana katika uwakilishi wa kisiasa.

Alisema chama hicho kimetoa makataa ya siku 60 kwa jopo la maridhiano la BBI kukamilisha vikao vyake kitaifa na kuwasilisha ripoti itakayojumuisha maoni ya wananchi kuhusu marekebisho ya Katiba yanayostahili.

Wiki iliyopita, Chama cha ODM kilitoa sababu mbalimbali za kupinga mswada huo, ikiwemo kwamba haujatoa pendekezo kuhusu mfumo wa uongozi utakaoleta nafasi ya Waziri Mkuu mwenye mamlaka makubwa ya kuongoza taifa.