Habari Mseto

Kesi ya Linturi na mkewe ipeperushwe moja kwa moja – Korti

September 2nd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA inayosikiza kesi ya talaka kati ya Seneta wa Meru Mithika Linturi na mkewe Maryanne Kitany Jumatatu ilikataa kuwafurusha wanahabari kupeperusha ushahidi moja kwa moja.

Hakimu mkuu Peter Gesora , alisema, wahusika katika kesi hiyo wanataka umma ujue sababu za kutalikiana, na tawi la Nairobi la chama cha wanasheria nchini (LSK) hakina msingi wowote kisheria kuomba korti izime kupeperushwa kwa ushahidi katika kesi hiyo.

Akiwasilisha ombi kesi hiyo iendelee kutangazwa, mawakili Dunstan Omari na Muthomi Thiankolu walisema mwenyekiti wa tawi la Nairobi la LSK Charles Kanjama alipotoka kutaka wanahabari wazuiliwe kuwaarifu umma kinachojiri.

“Tumeona habari katika mitandao katika mitandao kuwa LSK inaomba kesi ya Bi Kitany iendelezwe faraghani,” alisema Bw Omari.

Bw Thiankolu alisema sheria ni kwamba wahusika wako huru kuendeleza kesi yao adharani ama faraghani.

Wakili huyo alisema mteja wake pamoja na Bw Linturi ni watu wazima wanaojua umuhimu wa kufanya kesi hadharani.

Mahakama iliamuru wanahabari waendelee na jukumu lao la kupeperusha kesi hiyo .

Bw Gesora alisema mahakama inaelewa sheria na itatekeleza jukumu lake barabara.