Michezo

Kesi ya malipo duni ya wanasoka wanawake timu ya taifa ya Amerika yatupwa

May 2nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LOS ANGELES, AMERIKA

OMBI la timu ya taifa ya soka ya wanawake nchini Amerika la kutaka kulipwa kiwango sawa cha mshahara na wenzao wa kiume limefutiliwa mbali na mahakama kuu.

Kesi inayohusu madai kwamba kikosi cha wanawake hupokezwa malipo duni zaidi ikilinganishwa na vikosi vingine vya wanaume katika michezo mbalimbali nchini Amerika iliwasilishwa kortini mwaka jana.

Jumla ya wachezaji 28 wa timu ya taifa ya wanawake ya USA walitia saini stakabadhi za kesi hiyo dhidi ya Shirikisho la Soka la Amerika (USSF).

Kwa mujibu wa Molly Levinson ambaye ni msemaji wa vikosi vyote vya soka ya wanawake nchini USA, USSF ilistahili kuwafidia wanasoka hao wa kike kima cha Sh7.4 bilioni ambazo hawajakuwa wakilipwa kwa mujibu wa kanuni mpya za ujira za 2019.

Licha ya kesi hiyo kutupwa, Levinson ameapa kwamba watakata rufaa dhidi ya maamuzi hayo ya hapo jana.

“Tumeshangazwa na kuvunjwa moyo. Ingawa hivyo, hatutakata tamaa. Tutazidi kupigania haki ya kupokezwa malipo sawa na wanasoka wa kiume ambao sidhani wameletea taifa la Amerika tija yoyote jinsi ambavyo kikosi cha wanawake kimefanya katika takriban mashindano yote ya haiba kubwa,” akasema Levinson.

Kesi hiyo inayolalamikia kubaguliwa kwa wanasoka wa kike katika kiwango cha marupurupu ya usafiri, makazi na bima ya afya, itafikishwa mbele ya jaji wa Mahakama ya Rufaa jijini Los Angeles, Gary Klausner mnamo Juni 16, 2020.

Mahakama Kuu hapo jana iliamua kwamba: “Kikosi cha wanawake kimelipwa kiasi kikubwa zaidi cha fedha za jumla kutokana na wingi wa mafanikio yake katika mashindano mbalimbali. Tuzo za kifedha pekee ambazo zimetolewa kwa timu ya wanawake ya USA ni zaidi ya maradufu ya mishahara ambayo kikosi cha wanaume kimewahi kupata katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.”

Timu ya taifa ya soka ya wanawake nchini USA ilijinyakulia taji la Kombe la Dunia kwa mara ya nne mfululizo mwaka jana. Isitoshe, inajivunia kunyanyua nishani ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki mara tano.

Kwa upande wake, mvamizi Megan Rapinoe ambaye alitawazwa Mchezaji Bora na Mfungaji Bora katika fainali za Kombe la Dunia mwaka jana alisema, “Hatuchoka kudai haki na kupigania usawa.”

Kauli yake ilishadidiwa na mshambuliaji mwenzake katika timu ya taifa, Alex Morgan aliyesema, “vitisho havitaua ari yetu wala kuzima ndoto ya kupigania haki kwa minajili ya vizazi vijavyo.”

Aliyekuwa Rais wa USSF, Carlos Cordeiro alijiuzulu mnamo Machi 2019 baada ya kesi hiyo ya timu ya taifa ya wanawake ya USA kuwasilishwa mahakamani.

Kabla ya kuvaana na Japan katika kivumbi cha kuwania ubingwa wa taji la kipute cha SheBelieves mnamo Machi 12, 2020, wanasoka wa timu ya taifa ya USA waliandamana huku wakivalia jezi zao ndani-nje ili kuficha nembo za kikosi hicho.

Timu ya taifa ya soka ya wanaume ya USA iliwahi kutinga robo-fainali a Kombe la Dunia mnamo 2002. Ufanisi wao mkubwa zaidi katika ulingo wa soka ni kukamilisha fainali za Kombe la Dunia katika nafasi ya tatu mnamo 1930 mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.