Habari

Kesi ya mauaji anayokabiliwa nayo Gavana Obado yaahirishwa

October 10th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KESI ya mauaji anayokabiliwa nayo Gavana wa Kaunti ya Migori Okoth Obado na washukiwa wengine wawili iliahirishwa Jumatano kwa sababu jaji anayefaa kuisikiza alikuwa anasikiliza kesi nyinyine.

“Itabidi kesi hii iahirishwe kwa sababu Jaji Jessie Lesiit anayefaa kuisikiza yuko na kesi nyingine,” Jaji Stellah Mutuku aliwaeleza mawakili Jaji mstaafu Nicholas Ombija, Kioko Kilukumi na Nelville Amolo wanaowawakilisha washtakiwa.

Jaji Mutuku aliwaamuru washtakiwa wafike mbele ya Jaji Lesiit mnamo Oktoba 23, 2019, kwa maagizo zaidi.

Mahakama iliwataka washtakiwa hao ambao ni Gavana Obado, aliyekuwa msaidizi wake Michael Oyamo na Casper Obiero.

Wote wamekana kumuua aliyekuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo Sharon Otieno na mwanawe ambaye hakuwa amezaliwa.

Watatu hao walikanusha mashtaka dhidi yao na waliachiliwa kwa dhamana.

Marehemu alikuwa mpenziwe Obado.

Shtaka linasema mwanafunzi huyo aliuawa kinyama mnamo Septemba 3, 2018.

Sharon alikuwa na mimba ya miezi saba alipouawa na maiti yake na mwanawe zikaachwa msituni.

Upande wa mashtaka umesema kuwa Sharon; aliyekuwa na umri wa miaka 26 aliuawa katika eneo la Owade, Rachuonyo, Kaunti ya Homa Bay.

Mauaji ya Sharon yalisababisha maandamano ya wanafunzi wa chuo kikuu na wanaharakati huku wakiomba haki ifanywe.