Habari Mseto

Kesi ya mauaji dhidi ya Onyancha kusikizwa upya

July 31st, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu Jumatatu iliamuru kesi ya mshukiwa wa mauaji aliyeungamana kwa polisi aliwaua wanawake 19 na alikuwa amepanga kuwaua wanawake 100 ianze kusikizwa Novemba 19 mwaka huu.

Philip Ondara Onyancha alitiwa nguvuni miaka tisa iliyopita na kushtakiwa kwa mauaji ya wanawake na mvulana.

Kabla ya kushtakiwa mshukiwa huyu aliwaongoza maafisa wa Polisi katika Lojing mbali mbali Jijini Nairobi na miji mingine ambapo aliwaua wawanawake na kunywa damu yao baada ya kuwabaka.

Jaji Jessie Lesiit alitenga siku hiyo baada ya kuelezwa na kiongozi wa mashtaka Bw Moses Omirera kwamba kuna ripoti muhimu kuhusu utimamu wa ubongo wa Philip Ondara Onyancha ambayo haijapatikana katika faili ya mahakama.

Bw Omirera alimweleza Jaji Leesit kuna ripoti ya mtaalam wa tiba za akili Dkt Fredrick Owiti aliyempima Onyancha na kupendekeza akipatikana na hatia azuiliwe kwa hisani ya Rais katika gereza maalum mbali na umma  kwa vile “ anaugua maradhi ya ubongo ambayo yanapompata huwa anaingiwa na hamu na shauku kuu ya kuu ya kuwabaka wanawake, kuwaua na kunywa damu yao.”

Bw Omirera alimweleza Jaji Leesit kuwa ripoti  hiyo ilikuwa imetolewa mbele ya Jaji James Wakiaga aliyetamatisha mapema mwaka huu kesi ya Onyancha na kuamuru ianze kusikizwa upya.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema mashahidi 15 wameorodheshwa kutoa ushahidi dhidi ya Bw Onyancha wakiwamo wataalam wawili wa tiba za mardhi ya akili/ubongo.

Naibu wa msajili wa idara ya kuamua kesi za uhalifu alimteua wakili mwingine kumtetea Bw Onyancha  badala ya wakili Paul Muite.

Bw Muite alikuwa ameulizwa na Jaji mstaafu Nicholas Ombija amwakilishe Bw Onyancha.

Mshtakiwa anakabiliwa na shtaka la kumuua Catherine Chelangat  mnamo Novemba 22, 2008 katika mtaa wa Karen/Lang’ata kaunti ya Nairobi.

Bw Onyancha aliungama kwa polisi jinsi alivyokuwa kuwa akiwaua wanawake na kuficha miili yao.

Jaji Leesit alimwamuru Bw Omirera atafute barua hiyo ya Dkt Owiti na kumkabidhi wakili aliteuliwa kumtetea Bw Onyancha.

Na wakati huo huo Bw Onyancha aliomba aachuliwe kwa dhamana akisema “ nimekuwa gerezani karibu miaka kumi naomba uaniachilie kwa dhamana nifanye kesi nikiwa nje.”.

Ombi hilo lilipingwa na Bw Omirera akisema mshtakiwa anatakiwa kuwasilishwa ombi hilo kirasmi ndipo afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) iwasilishe tetezi za kuipinga.

“ Kesi hii itatajwa mnamo Septemba 20 wakati mshtakiwa atawasilisha ombi la kuachiliwa kwa dhamama naye Bw Omirera aeleze ikiwa amepata ripoti hiyo ya Dkt Owiti,” aliamuru Jaji Leesit.