Habari Mseto

Kesi ya mauaji ya wakili Kimani yaahirishwa

October 20th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Jumatatu iliahirisha kusikizwa kwa kesi ya mauaji ya wakili Willie Kimani pamoja na mteja wake miaka minne iliyopita, baada ya mmoja wa washukiwa watano kuambukizwa maradhi ya Covid-19.

Akiahirisha kesi hiyo, Jaji Jessie Lesiit, alisema Bw Stephen Cheburet Morogo, ameugua Covid-19 na kesi haingeweza kuendelea kama hayuko.

Jaji Lesiit aliombwa na wakili Cliff Ombeta anayemwakilisha Bw Morogo aahirishe kesi hiyo kumwezesha mteja wake kuwa kortini ushahidi ukitolewa.

Hata hivyo, Bw Morogo alipewa fursa kupitia mawasiliano ya video akiwa gereza kuu la Kamiti kuwasiliana na Jaji Lesiit.

Bw Morogo alijieleza akisema, “Mheshimiwa naomba uahirishe kesi hii kwa siku kadhaa ndipo nipimwe kama nimepona corona Oktoba 22,2020. Ripoti ya ukaguzi wangu kubaini kama nimepona itawasilishwa kortini na idara ya magereza.”

Mshtakiwa huyo alisema kwamba amepimwa mara nne na kila mara anapatikana bado hajapona.

Mahakama ilielezwa mbali na Bw Morogo pia washtakiwa wenzake, Fredrick ole Leliman na Slyvia Wanjiku Mwangi pia waliambukizwa ugonjwa huo lakini wamepona.

“Naomba hii mahakama izingatie mawasilisho ya mshtakiwa mwenyewe kwamba apewe muda apone ndipo afike kortini kujitetea,” alisema Bw Ombeta.

Vile vile, korti iliamuru Bi Mwangi azuiliwe katika kituo cha polisi cha Kileleshwa kufanyiwa ukaguzi wa kimatibabu.

Jaji Lesiit aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 26, 2020 kuwezesha Bw Morogo kupata nafuu.

Na wakati huo huo, mahakama iliamuru washtakiwa wawasilishe upya ombi lao la kuachiliwa kwa dhamana tena.