Habari Mseto

Kesi ya mfyonza damu Onyancha kusikizwa upya

April 5th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MAHAKAMA Kuu Alhamisi ilisimamisha kwa muda kesi iliyomkabilia Philip Onyancha aliyekabiliwa na tuhuma ya kuwaua watu kisha kuwafyonza damu, na kuamuru isikizwe upya.

Watu wengine wawili walioshtakiwa na Onyancha waliachiliwa huru.

Jaji James Wakiaga alikosoa upande wa mashtaka, akisema kesi hiyo ilipaswa kuendeshwa chini ya sehemu ya 162 ya Sheria ya Uhalifu kwa sababu ilikuwa wazi tangu mwanzo kwamba Onyancha alikuwa na tatizo la kiakili.

Watatu hao walishtakiwa chini ya sehemu ya 166 ya sheria ya uhalifu.

Jaji aliamuru kwamba faili ya kesi hiyo ipelekwe kwa Mkuu wa Kitengo cha Mahakama kinachoshughulika na kesi za Uhalifu Jaji Jessie Lesiit ili kesi hiyo isikizwe tena.

Wakati wa mawasilisho ya mwisho mapema mwaka huu, upande wa mashtaka uliitaka korti kumpata mshukiwa na hatia ya kuua kimakusudi licha ya kuwa na akili punguani.

Kulingana na mwendesha mshtaka huyo, Bw Onyancha ni mtu hatari lakini anahitaji kusaidiwa.

Akiachiliwa huru, Bw Omirera aliongeza, mshtakiwa huyo anaweza kutekeleza vitendo vingine vya uhalifu aina hiyo, haswa akiwalenga wanawake.

Bw Omirera aliambia mahakama kwamba kulikuwa na ripoti tatu za uchunguzi wa kiakili iliyowasilishwa kortini, mmoja ya ripoti hiyo ikiwasilishwa na Dkt Owiti.

Kulingana na ripoti ya Dkt Owiti, kuna uwezekano mkubwa Onyancha angetekeleza makosa mengine kama hayo aliyoshtakiwa kwayo.

Kulingana na ripoti ya kwanza iliyotolewa siku chache baada ya Onyancha kukamatwa, ilibainika kuwa alikuwa muuaji sugu na alifaa kushtakiwa.

Lakini alipofika mahakamani kwa mara ya kwanza mnamo Juni 2010, wakili wake Peter Simani aliiambia mahakama kwamba Bw Onyancha alikuwa na tatizo la kiakili na alifaa kuchunguzwa.

Jopo la madaktari watatu walimfanyia uchunguzi kwa mara nyingine.

Ilibainika kuwa Onyancha alikuwa na tatizo la kiakili lakini ripoti hiyo haikuwa kamilifu.

Pande husika katika kesi hiyo iliitisha uchunguzi wa tatu, uliobaini kuwa Bw Onyancha alikuwa hatari na huenda angetekeleza uhalifu mwingine.

Ilidaiwa kuwa Bw Onyancha alikiri kuwaua wanawake 19 na watoto.

Alikuwa ameshtakiwa na makosa matatu ya mauaji kwa kukusudia akiwa pamoja na Tobias Nyabuhanga Aradi na Douglas Obiero Makori.

Walikana madai kuwa mnamo Aprili 14, 2014 mtaani Dogoretti Nairobi waliua mtoto mwenye umri wa miaka tisa Anthony Njirwa Muiruri.