Michezo

Kesi ya rais wa PSG na kinara wa FIFA kuanza Septemba

June 6th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

RAIS wa Paris Saint-Germain (PSG), Nasser Al-Khelaifi na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Jerome Valcke watafunguliwa mashtaka ya ufisadi mnamo Septemba 2020.

Kesi ya wawili hao inahusishwa na kukiukwa kwa haki nyingi za vyombo vya habari wakati wa kupeperushwa kwa michuano mbalimbali ya FIFA.

Kesi hiyo pia inamhusisha mwanamume wa tatu, ambaye hajatajwa jina, na inahusu madai ya usimamizi mbaya, uchochezi na matumizi ya stakabadhi ghushi katika utolewaji wa tenda mbalimbali.

Mashtaka na hatimaye hukumu dhidi ya watatu hao itatolewa katika jiji la Bellinzona, Uswizi.

Hata hivyo, mawakili wa Khelaifi wamepuuzilia mbali madai yote dhidi ya mteja wao na kusisitiza kwamba hayana msingi wala mashiko.

Aidha, mawakili hao wamewasilisha malalamishi rasmi mahakamani wakipinga kuendelea kwa mashtaka dhidi ya Khelaifi ambaye alianza tu kushtumiwa baada ya madai mengi dhidi yake kuanikwa mitandaoni.

Al-Khelaifi ambaye pia ni mwenyekiti wa BeIN Media anashtumiwa kutoa zawadi mbalimbali kama hongo kwa Valcke ili kumwezesha kupata haki za kupeperusha runingani mashindano mengi ya haiba kubwa ya soka, zikiwemo fainali za Kombe la Dunia.

Mnamo Februari 2020, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu nchini Uswizi ilisema kwamba ilikuwa imemwondolea Al-Khelaifi mashtaka ya kutoa rushwa ili kushawishi maamuzi ya atakayekuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia za 2026 na 2030.

Wakati huo, FIFA ilisisitiza kwamba ilikuwa imeafikiana na bwanyenye huyo mzawa wa Qatar kuhusu haja ya kesi hiyo kusuluhishwa nje ya mahakama.

Kwa upande wake, Valcke amedaiwa kutumia mamlaka yake katika usimamizi wa FIFA kati ya 2013 na 2015 kushawishi kutolewa kwa haki za kupeperushwa runingani kwa mashindano mbalimbali ya haiba kubwa ya FIFA nchini Italia na Ugiriki pamoja na fainali za Kombe la Dunia za zilizoratibiwa kufanyika kati ya 2018 na 2030.

Kampuni ya Sportunited LLC inayomilikiwa na Valcke inadaiwa pia kupokea hongo ya hadi Sh1.6 bilioni ili kughushi baadhi ya stakabadhi za kutolewa kwa tenda mbalimbali za FIFA katika juhudi za kufanikisha maandalizi ya fainali za Kombe la Dunia za 2018 na 2022.

Valcke ambaye aliwahi kufanya kazi na rais wa zamani wa FIFA, Sepp Blatter kati ya 2003 na 2015, tayari amepigwa marufuku ya miaka 10 kwa kukosa kushirikiana na wapelelezi waliokuwa wakichunguza madai ya kuuzwa kwa tiketi za fainali za Kombe la Dunia kwa bei ya juu zaidi kupita kiasi.