Habari Mseto

Kesi ya Sonko isikizwe na mahakama ya ufisadi, aamuru jaji

November 22nd, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu imeamuru kesi iliyowasilishwa na Gavana wa Nairobi Mike Sonko akipinga kuchunguzwa na Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) isikizwe na idara inayoshughulikia kesi za ufisadi na uporaji mali ya umma.

Akikataa kesi hiyo ya Gavana Sonko isikizwe na kitengo cha mahakama kuu cha kutetea haki za binadamu , Jaji James Makau alisema mwongozo aliotoa Jaji Mkuu (CJ) David Maraga ni kuwa kesi zote kuhusu ufisadi zisikizwe na kuamuliwa na kitengo cha mahakama kuu kinachoamua kesi zinazohusu ufisadi na uporaji wa mali ya umma.

Jaji Makau alikubaliana na wakili Paul Muite anayemwakilisha Mkurugenzi wa Uchunguzi wa EACC Bw Abdi A Mohamud Abdi kwa ombi hilo la Sonko lapasa kusikizwa na kuamuliwa na Jaji Hedwig Ong’undi wa idara ya mahakama kuu ya kuamua kesi za ufisadi.

Bw Muite alimweleza Jaji Makau kuwa kesi hiyo ya Sonko itasikizwa na kuamuliwa kwa upesi katika idara ya ufisadi na uporaji wa mali ya umma.

Jaji Makau alisema Jaji Maraga alitenga idara katika mahakama kuu kuamua kesi za ufisadi na masuala ya kiuchumi.

“Ili malalamishi ya Gavana Sonko yasikizwe na kuamuliwa haraka nitapeleka kesi hii mbele ya Jaji Ong’undi mnamo Novemba 22, 2019 aitengee siku ya kusikizwa,” aliamuru Jaji Makau.

Wakili Paul Muite akimtetea mkurugenzi wa uchunguzi wa EACC. Picha/ Richard Munguti

Akiwasilisha ombi hilo mbele ya Jaji Makau, wakili Cecil Miller anayemwakilisha Sonko alipinga ombi EACC ikimchunguza kwa madai alikuwa ametoboa siri Bw Mohamud akishirikiana na watu wengine waliuza jengo la Integrity Centre , iliyo makao makuu ya EACC kwa bei ya Sh1.5bilioni.

Pia Gavana huyu amesema anaonewa kwa vile alifichua Bw Mohamud akishirikiana na watu wengine alinyakua uwanja uliotengewa shughuli za umma kwa bei ya Sh42.5milioni katika mtaa wa Mugoya, South C Nairobi.

Akisema Bw Sonko , Bw Miller alisema Gavana huyu anaomba achunguzwe na kushtakiwa iwapo yuko na hatia kama wananchi wengine wa kawaida lakini akasema “ achunguzwe na kitengo kingine cha serikali na wala sio EACC.”

Bw Miller alisema Sonko anadai anaonewa na Bw Mohamud.

Katika ushahidi aliowasilisha katika Mahakama kuu Sonko amedai Mohamud alishirikiana na watu wengine kuuza jengo la Integrity Centre kwa bei ya Sh1.5bilioni na kunyakua ardhi ya umma katika mtaa wa Mugoya , South C Nairobi.

Sonko amedai kuwa habari zilizowasilishwa kwa Mohamud alizitumia kujiandikishia umiliki wa ardhi hiyo pamoja na rafikiye Isaack Abdullahi Ibrahim na hatimaye kuiuza kwa bei ya Sh42,500,000.

Wakili J K Mwangi alisimamia kuuzwa kwa ardhi hiyo kati ya Kibira na Isaack Abdullahi Ibrahim. Mnamo Novemba4 2014 mawakili wa Isaack Iseme, Kamau & Maema Advocates walimkabidhi Kibira Sh38,250,000 kupitia Benki ya I & M.

Sonko amesema kuwa mnamo Desemba 23, 2014 afisa mkuu katika kaunti ya Nairobi Stephen Gathuita Mwangi Sh10,350,000.