Habari Mseto

Kesi ya uchochezi dhidi ya Muthama na Aladwa kutajwa Novemba

June 5th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Kamkunji George Aladwa na aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama wanaokabiliwa na mashtaka ya uchochezi na udunishaji wa afisi ya Rais Jumatano walihoji sababu kesi zinazowakabili hazijasitishwa.

Wakili Dkt John Khaminwa anayewatetea wanasiasa hao alimweleza hakimu mkuu Francis Andayi kuwa kesi za wanasiasa wengine walioshtakiwa wakati mmoja na Mabw Aladwa na Muthama zimetamatishwa.

“Nashangaa sababu kesi dhidi ya Mabw Aladwa na Muthama hazijatamatishwa ilhali uhusiano mwema ulirudishwa kati ya Jubilee na vyama vya Upinzani,” alisema Dkt Khaminwa.

Wakili huyo alimweleza hakiwa atawasilisha kesi katika mahakama kuu kuhoji sababu za kutositishwa kwa kesi dhidi ya Mabw Aladwa na Muthama ilhali handisheki imesuluhisha masuala na tofauti kuu kati ya muungano wa Nasa na Jubilee.

Wawili hao wameshtakiwa kwa kuchochea uhasama na kudunisha afisi ya Rais walipohutubia mikutano katika bustani ya Uhuru Park.

Andayi aliorodhesha kesi hiyo kutajwa Novemba 2019 kuipa afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma fursa ya kuwasiliana mamlaka ya maridhiano.