Kesi ya ufisadi ya Obado na wanawe kuendelea Nairobi

Kesi ya ufisadi ya Obado na wanawe kuendelea Nairobi

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu jana ilikataa kuhamisha kesi ya ufisadi wa Sh73milioni dhidi ya Gavana Okoth Obado , wanawe na wafanyabiashara wengine kusikizwa na kuamuliwa katika mahakama ya Migori.

Akitupilia mbali ombi hilo lililowasilishwa na mmoja wa washukiwa walioshtakiwa pamoja na Bw Obado , Jaji James Wakiaga alisema washtakiwa wengine 12 wanataka kesi iendelee katika mahakama ya Milimani Nairobi.

Mshukiwa huyo , Bw Joram Opala Otieno kupitia kwa wakili George Kithi alidai mahakama ya Nairobi haipasi kuamua makosa yaliyofanyika katika kaunti ya Migori ilhali kuna korti zilizo na uwezo wa kuamua kesi hizo.

“Ni mwongozo na utaratibu wa kisheria kwamba makosa yaamuliwe eneo yalimofanyika,” alisema Bw Kithi.

Akiwasilisha ombi hilo ,Bw Otieno alisema makosa anayoshtakiwa nayo yalitendeka katika kaunti ya Migori na “ ingelifaa tu kesi hiyo iamuliwe huko.”

Alisema kuhamishwa kwa kesi hiyo hadi kaunti ya Nairobi kumetatiza mambo mengi miongoni mwao gharama za usafiri na malazi kila wakati kesi hiyo inapotajwa.

Bw Otieno aliomba Jaji Wakiaga aamuru kesi hiyo ipelekwe kusikizwa katika mahakama ya Migori.

“Tunagharamika sana kusafiri kila wakati kutoka kaunti ya Migori hadi Nairobi,” mshukiwa huyo alieleza mahakama.

Jaji Wakiaga alisema kesi inaweza sikizwa na mahakama yoyote.

Alisema afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma haikukosea ilipoamuru kesi isikizwe Nairobi.

Na wakati huo huo hakimu mkuu Bw Lawrence Mugambi anayesikiza kesi hiyo alisema ataitengea muda kesi hiyo kusikizwa katika muda wa mwezi mmoja ujao.

Alikataa ombi la kusitisha kusikizwa kwa kesi hiyo hadi mahakama ya rufaa iamue ikiwa itaagiza kesi hiyo ipelekwe Migori au la.

“Hii mahakama imekamilisha kuhoji taratibu zote kabla ya kesi kuanza kusikizwa,” alisema Bw Mugambi.

You can share this post!

Mshtakiwa ageuzwa shahidi katika kesi ya ukwepaji ushuru

Wakala akana kuiba Sh11 milioni za bima