Kimataifa

Kesi ya uhalifu dhidi ya Trump yaanza kusikizwa baada ya kuahirishwa mara kadhaa

April 16th, 2024 1 min read

Na MASHIRIKA

NEW YORK, Amerika

KESI ya uhalifu dhidi ya Rais wa zamani wa Amerika Donald Trump ilianza Jumatatu jijini New York na kuhudhuriwa na kiongozi huyo.

Trump anakabiliwa na makosa ya kughushi rekodi za kibiashara katika njama yake ya kuficha madai ya mahusiano yake kimapenzi na mwigizaji filamu za ngono Stormy Daniel.

Ilidaiwa alifanya hivyo ili asilaumiwe kwa kuvunja sheria za uchaguzi wa urais alioushinda mwaka wa 2016.

Trump, anayepania kuwania urais kwa mara nyingine Novemba mwaka huu, kwa udhamini wa chama cha Republican, ndiye rais wa kwanza wa zamani wa Amerika kuwahi kushtakiwa kwa uhalifu.

Kesi hiyo ya kihistoria inaongozwa na Jaji Juan Merchan katika Mahakama ya Manhattan.

Akiongea na wanahabari baada ya kusimamishwa kwa shughuli ya uteuzi wa wasimamizi wa kesi hiyo, Trump alisema hivi: “Kesi zote ni za Biden (Rais Joe Biden), mwajua hilo, sawa? Najivunia kuwafanyia kazi Waamerika. Muwe na wakati mwema kufuatilia matukio.”

Wachanganuzi wa siasa wanasema kesi hiyo itafuatiliwa kwa karibu kuonekana kama haki itatendeka, kwa sababu ni ya kwanza ya uhalifu dhidi ya rais wa zamani.

Calvin Dark, mchanganuzi wa masuala ya siasa anasema hivi: “Naamini kufikia sasa majaji na waendesha mashtaka wamefanya kazi nzuri. Hii ni katika jitihada za kuhakikisha kuwa Trump anatendewa jinsia Mwamerika mwingine katika hali hiyo angetendewa.”

Kuhusu iwapo kesi hiyo itamwathiri Trump kisiasa, Gavana wa New Hampshire Chris Sununu anasema hivi: “Sidhani kama Rais huyu wa zamani ataathirika kisiasa kuelekea uchaguzi wa urais wa Novemba. Kwa hakika kesi hiyo itamjenga kwani wapiga kura wataona kwamba anadhulumiwa.”

Aidha, Gavana Sununu aliondoa hofu kwamba kesi hiyo itavuruga kampeni za Trump akisema “mikutano yote ya kampeni za mgombeaji huyu wa urais itaendelea ilivyopangwa.”