Habari Mseto

Kesi yako ilikuwa stori za ‘jaba’, korti yaambia Ann Njeri wa mafuta ya 17b

March 26th, 2024 2 min read

NA BRIAN OCHARO

MAHAKAMA imetupilia mbali kesi ambapo mfanyabiashara Ann Njeri Njoroge alidai umiliki wa tani 100, 000 za dizeli yenye thamani ya Sh17 bilioni alizodaiwa kuingiza nchini Oktoba 2023.

Jaji wa Mahakama Kuu mjini Mombasa, Kizito Magare, badala yake amemshauri mwanamke huyo kujiepusha na kutazama filamu za wizi wa pesa.

Hii ni baada ya Jaji huyo kuamua kuwa mwanamke huyo alishindwa kutoa ushahidi kuthibitisha kuwa aliwahi kuingiza mafuta ya aina hiyo nchini.

“Ninaweza kuelezea kuwa madai ya mlalamishi lilikuwa jaribio la uwongo. Mlalamishi anapaswa kuacha kutazama sinema nyingi, haswa ‘wizi wa pesa,’” alisema Jaji Kizito.

Mahakama pia ilibaini kuwa stakabadhi ambazo mwanamke huyo aliwasilisha kupitia kampuni yake, Ann’s Import and Export Enterprises Ltd, ziliacha shaka kwamba hakuna tone la mafuta lingeweza kuondoka katika Ufalme wa Saudi Arabia.

Jaji aligundua kuwa hati zote ambazo Bi Njoroge aliwasilisha hazithibitishi ununuzi, uingizaji au mahitaji ya Dizeli EN 590.

Ushahidi uliowasilishwa mahakamani unaonyesha zaidi kuwa mafuta yaliyopakuliwa ni Gas oil 50ppm Automotive Gas Oil (AGO) na sio Dizeli EN 590.

Zaidi ya hayo, maelezo ya Halmashauri ya Ushuru nchini (KRA) yalionyesha kuwa bidhaa iliyoagizwa nchini ilikuwa ni AGO.

Bi Njoroge aliwasilisha kesi hii mwaka jan, 2023,  akilalamika kwamba alichezwa katika mkataba wa mafuta alioleta kutoka Jeddah, shehena hiyo ilipofika bandari ya Mombasa Oktoba mwaka jana.

Hata hivyo, alipopewa nafasi ya kutoa ushahidi wa kuunga mkono madai yake ya umiliki wa shehena iliyowasili nchini kwa meli ya MV Haigui, ushahidi alioutoa uliiacha mahakama ikihoji ni kwa nini aling’ang’ania umiliki wa shehena hiyo.

“Dizeli aina hiyo haikuwahi kufika nchini. Bidhaa ambazo Galana Energies Ltd ilinunua ni tofauti na zile zinazodaiwa na Ann’s Import and Export Enterprises ltd,” alisema Jaji Magare.

Mahakama ilibaini kuwa mlalamishi (Ann’s Import and Export Enterprises ltd) hakuwa na miundombinu inayohusiana na meli na mizigo na kwamba shehena iliyokuwa ikipigana na Galana Energies Ltd ilikuwa tofauti.

“Wanapaswa kuwasilisha kesi yao huko Jeddah ambapo wanaweza kuwa wamepotoshwa au vinginevyo walianzisha mpango wa kuiba mafuta. Dizeli EN590 haijafika na haikuwa ndani ya meli ya Haigui. Hii ni kesi ya kutupiliwa mbali na haiwezi kuokolewa kwa kufanyiwa marekebisho ya aina yoyote,” alisema Kizito.

Bi Njoroge ambaye ni mkurugenzi pekee wa kapmuni hiyo ya Anns Import and Export Enterprise LTD alishtaki kampuni ya Galana Energies Ltd, Halmashauri ya Bandari nchini (KPA ) na KPC kuhusu shehena hiyo. Kampuni ya Galana Energies Ltd ilidai umiliki wa mizigo hiyo ikibaini kuwa kampuni ya Bi Njoroge haijaidhinishwa kushughulikia uagizaji na usambazaji wa bidhaa za petroli nchini.

Kulingana na Bi Njoroge, alikuwa ameagiza tani 100, 000 za mafuta zilizopakiwa kwenye meli ya Haigui kabla ya kunyanganywa mzigo meli ilipowasili nchini.

Mahakama ilibaini kuwa Bi Njoroge hakutoa ushahidi wowote wa kuonyesha kuwa alilipia, kupata, kuagiza , kandarasi ya ununuzi, au chochote ambacho mahakama inaweza kutegemea.