Habari Mseto

Kesi za ufisadi za Sh224 bilioni zimekwama kortini – Haji

November 11th, 2020 1 min read

Na BENSON MATHEKA

Kesi 135 za ufisadi zinazohusu uporaji wa Sh224 bilioni pesa za umma, zinaendelea katika mahakama tofauti nchini, ripoti ya hivi punde ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji imefichua.

Ripoti hiyo aliyomkabidhi Rais Uhuru Kenyatta Jumatatu inasema kwamba, baadhi ya kesi hizo zilizowasilishwa kati ya 2017 na Juni 2020, zinahusu maafisa wa serikali, wakiwemo mawaziri, magavana, makatibu wa wizara, wakurugenzi wa mashirika ya serikali, wabunge na madiwani.

“Kesi 53 kati ya zilizowasilishwa kortini zinahusu maafisa wakuu wa serikali wakiwemo mawaziri na makatibu saba, magavana na maafisa wakuu wa kaunti zao 11, wakurugenzi 22 wa mashirika tofauti na wabunge saba,” inasema ripoti hiyo.

Miongoni mwa mawaziri walioshtakiwa kwa ufisadi kati ya 2017 na 2020 ni aliyekuwa waziri wa Uchukuzi Michael Kamau, aliyekuwa Waziri wa Michezo Hassan Wario na aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich.

Baadhi ya makatibu wa wizara walioshtakiwa ni Lilian Omollo (utumishi wa umma), Richard Lesiyampe (Kilimo) na Peter Mangiti ( ugatuzi). Mangiti aliachiliwa na mahakama kutokana na ukosefu wa ushahidi.

Bw Haji anasema tangu achukue usukani katika afisi ya mashtaka ya umma, idadi ya kesi zinazofaulu kortini imeongezeka mno. “Idadi ya kesi za kawaida zinazofaulu na washtakiwa kupatikana na hatia imeongezeka kutoka asilimia 90.2 mwaka wa 2017 hadi asilimia 92.5 kufikia Juni mwaka huu. Vile vile, idadi ya kesi za ufisadi zinazofaulu imeongezeka kutoka asilimia 37.4 hadi asilimia 63 katika kipindi hicho,” anasema katika ripoti hiyo.

Anasema hii inatokana na mikakati aliyoweka kuimarisha utendakazi wa afisi hiyo ili kuhudumia umma.Kulingana na Bw Haji, licha ya kupiga hatua kubwa katika utendakazi wake, afisi hiyo inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa wafanyakazi.Kwa sasa, afisi hiyo ina wafanyakazi 996 ilhali inapaswa kuwa na wafanyakazi 2156 ili kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Bw Haji alikiri kwamba waendesha mashtaka wanakabiliwa na changamoto kuongoza kesi za ufisadi ambazo zinahusu stakabadhi nyingi kama ushahidi na zinahitaji utaalamu na tajiriba ya hali ya juu.