Habari Mseto

Kesi za waliouawa na polisi bado zinajikokota -IPOA

January 23rd, 2020 2 min read

Na PETER MBURU

ZAIDI ya mwaka mmoja tangu mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Leeds, Carilton Maina alipouawa na polisi, kesi yake ingali inajikokota na haijafika kortini, licha ya uchunguzi kukamilika awali 2019.

Mamlaka Huru ya Usimamizi na Uangalizi wa Polisi (IPOA) jana ilisema japo iliwasilisha faili ya kesi ya mwanafunzi huyo kwa Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) mnamo Aprili mwaka jana, kesi hiyo haijafikishwa kortini.

Hali ni sawa na hiyo kuhusu kesi ya mtoto wa miaka miwili, Dan Githinji, ambaye alipigwa risasi na polisi waliokuwa wakitafuta hongo kwa watengenezaji wa pombe haramu, katika mtaa wa Kahawa West, Nairobi.

“Bado tunasubiri washukiwa wafikishwe kortini kwani tulikamilisha uchunguzi na kuwasilisha faili kwa DPP,” mwenyekiti wa IPOA Anne Makori akasema jana.

Akiongea wakati wa kikao na wanahabari kutoa ujumbe kuhusu visa vinavyohusisha polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia ama polisi wenzao, Bi Makori alisema mamlaka hiyo imepokea malalamishi mengi kutoka kwa Wakenya, japo uchunguzi wa mengi kati yayo haujakamilika, na kuhusu yaliyokamilika, hayajafikishwa kortini.

“Hadi wakati wa mwisho tulipotoa habari, mamlaka hiyo imepokea malalamishi 13,618 na 1,518 kati yake yakachunguzwa. Tumewasilisha faili za malalamishi 180 kwa DPP, ambapo kesi 75 kati yake ziko kortini sasa,” Bi Makori akasema.

Makamishna wa IPOA walisema katika matukio mengi ambapo polisi wamehusika na uhalifu ama kupiga raia risasi, mashahidi wanahofia maisha yao ama kutishiwa, na hivyo hawajitokezi, jambo walilosema linafifisha uchunguzi.

IPOA aidha iliripoti kuwa miaka ya majuzi kumekuwa na mtindo wa polisi kuwaua wenzao, ama raia kuwajeruhi ama kuwaua polisi, ikisema ni suala ambalo pia inachunguza.

Hata hivyo, mamlaka yenyewe pia haina uwezo zaidi ya kuchunguza visa hivyo kisha kuwasilisha faili za kesi na mapendekezo kwa DPP ama Tume ya Huduma za Polisi (NPSC), kwani mapendekezo yake yasipotekelezwa, haifanyi lolote.

Majuzi, Rais Uhuru Kenyatta aliamrisha wizara ya Usalama wa Ndani kukoma kuwahamisha polisi wanaopatikana wakifanya uhalifu ama ufisadi, na badala yake kuwapiga kalamu.