Keter, Munyes wakasirisha maseneta kwa kudinda kufika mbele yao kujibu maswali kuhusu bei ya mafuta

Keter, Munyes wakasirisha maseneta kwa kudinda kufika mbele yao kujibu maswali kuhusu bei ya mafuta

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Kawi Charles Kater na mwenzake wa Mafuta na Madini John Munyes Jumanne walidinda kufika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Kawi kujibu maswali kuhusu ongezeko la bei ya mafuta wiki jana.

Akitoa sababu ya kutofika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Nyeri Ephraim Maina, Bw Keter alisema kuwa suala la bei ya mafuta haliko chini ya wizara yake bali ile ya mwenzake Bw Munyes.

Kwa upande wake waziri Munyes yuko nje ya nchi kwa ziara ya kikazi.

Kwenye barua kwa kamati hiyo kupitia afisi ya Karani wa Seneti Jeremiah Nyengenye, waziri huyo wa Mafuta aliomba kufika mbele ya kamati hiyo Jumatano juma lijalo.

Hata hivyo, maseneta wanachama wa Kamati hiyo waliwakaripia mawaziri hao wakiahidi kuwasilisha suala hilo katika kikao cha bunge lote ili kipendekeze adhabu kwa Mbw Keter na Munyes.

“Waziri Keter anapata wapi mamlaka na ujasiri wa kudai kuwa suala hili halihusu wizara yake? Tunafahamu kwamba bei ya juu ya mafuta na bei ya stima zinahusiana. Wananchi wanaumia na wanafaa kupunguziwa gharama ya mahitaji haya,” akasema Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.

“Waziri Munyes alifaa kukatiza safari yake ughaibuni na kuitikia mwaliko kutoka kwa maseneta kujadili suala hili lenye umuhimu wa kitaifa. Ukiongeza bei ya mafuta, bei ya kila bidhaa na huduma bila shaka hupanda,” akaongeza Bw Wetang’ula ambaye pia ndiye kiongozi wa Ford Kenya.

Kwa upande wake, Seneta wa Narok Ledama Olekina alilaumu Bunge la Kitaifa kutoka hatua yake ya kupitisha miswada iliyopendekeza nyongeza ya bei za bidhaa za mafuta nchini.

“Kwa mfano, ni sisi wabunge na maseneta tuliopitisha sheria ya Mafuta iliyochangia kuanzishwa kwa ada ya ustawi wa sekta ya mafuta,” akasema Bw Olekina.

Lakini wanachama wengine waliondoa Seneti katika wajibu wa kupitishwa kwa miswada inayohusiana na ushuru wakisisitiza kuwa wajibu huo uko mikononi mwa wenzao katika Bunge la Kitaifa.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa kamati hiyo Bw Maina alisema kuwa wao kama maseneta na bunge lote kwa ujumla hawatachoka kuendelea na kampeni yao ya kuhakikisha kuwa ushuru na ada zingine ambazo hutozwa mafuta zinapunguzwa.

“Tunaendeleza uchunguzi ili kubaini ni jinsi ipi tunaweza kuingilia suala hilo kisheria kwa manufaa ya wananchi wanaoumia wakati huu kutoka na majanga kama vile ukame na Covid-19,” akaeleza Seneta huyo wa Nyeri.

Bw Maina alisema kando na bei ya mafuta, bunge hilo la seneti pia litaingilia kati bei za juu za unga, sukari na bidhaa nyinginezo za kimsingi.

“Pia tutashinikiza karo za shule zipunguzwe kwa sababu wananchi wameumizwa zaidi,” akaeleza.

You can share this post!

Pigo kwa Liverpool baada ya kiungo Thiago Alcantara kupata...

Mfahamu Jarred Gillett ambaye sasa atakuwa refa wa kwanza...