Michezo

Kevin De Bruyne atawazwa Mchezaji Bora wa EPL

August 17th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO matata wa Manchester City, Kevin De Bruyne, 29, ametawazwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Nyota huyo mzawa wa Ubelgiji alipachika wavuni jumla ya mabao 13 msimu huu na kuwaongoza Man-City kukamilisha kampeni za EPL katika nafasi ya pili nyuma ya Liverpool waliotazwa mabingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.

De Bruyne alifikia pia rekodi ya 2002-03 ya aliyekuwa kigogo wa soka kambini mwa Arsenal, Thierry Henry kwa kuchangia jumla ya mabao 20 katika EPL msimu huu wa 2019-20.

Kwa ufanisi huo, De Bruyne anakuwa mchezaji wa tatu mzawa wa Ubelgiji baada ya Vincent Kompany na Eden Hazard kutia kutwaa taji la Mchezaji Bora wa EPL katika kipindi cha misimu tisa iliyopita.

Kompany ambaye kwa sasa ni beki na kocha wa Anderlecht nchini Ubelgiji, alitwaa taji hilo akivalia jezi za Man-City. Kwa upande wake, Hazard ambaye kwa sasa ni mwanasoka wa Real Madrid nchini Uhispania, alituzwa alipokuwa kiungo wa Chelsea.

Mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa EPL msimu huu alipatikana baada ya umma kushiriki upigaji kura kupitia mtandao wa Electronic Arts (EA) Sports. Kura hizo zilijumuishwa na za manahodha wote 20 wa klabu za EPL pamoja na zile za jopo la wataalamu wa soka.

De Bruyne aliwapiga kumbo mvamizi Danny Ings wa Southampton, fowadi Jamie Vardy wa Leicester City, kipa Nick Pope wa Burnley na wanasoka watatu wa Liverpool – Trent Alexander-Arnold, Jordan Henderson na Sadio Mane.

Mnamo Agosti 15, Jurgen Klopp wa Liverpool alitawazwa Kocha Bora wa EPL siku moja baada ya beki Alexander-Arnold kutuzwa Chipukizi Bora wa EPL katika msimu wa 2019-20.