Habari Mseto

Kevin Opiyo Oliech aaga dunia, marehemu ni kaka yake Dennis Oliech

August 16th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI wa zamani wa Mathare United, Kevin Opiyo Oliech ameagana dunia.

Opiyo, 33, ni kakaye mdogo nyota wa zamani wa Gor Mahia, Nantes ya Ufaransa na timu ya taifa ya Harambee Stars, Dennis ‘The Menace’ Oliech na mwanasoka Andrew Oyombe ambaye pia aliwahi kuchezea Harambee Stars na Gor Mahia.

Kifo cha Opiyo ambacho kimetokea Ujerumani alikokuwa wakati akijiandaa kusafiri hadi Amerika kwa matibabu zaidi, kimethibitishwa na kakaye Nixon Onywanda.

“Amekuwa akiugua saratani kwa kipindi cha miaka minne iliyopita. Amekuwa wa kutoka na kurudi hospitalini kwa miaka hiyo minne iliyopita. Alirejea humu nchini mwaka jana kabla ya kurudi tena Ujerumani,” akasema Onywanda.

Mbali na Mathare ambao walitawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya humu nchini mnamo 2008, Opiyo aliwahi pia kuvalia jezi za Ushuru FC, Thika United, Nairobi City Stars na mabingwa mara 11 wa Ligi Kuu ya KPL, Tusker.

Kimataifa, Opiyo aliwahi pia kucheza kikosi cha KFC Uerdingen 05 kinachoshiriki Ligi ya Daraja la tano nchini Ujerumani kisha kusajiliwa na Alemannia Aachen cha Daraja la Pili nchini humo kabla ya kuangika rasmi daluga zake.

Kifo cha Opiyo kinatokea miaka miwili baada ya kuaga kwa mama mzazi, Mary Auma Oliech mnamo Julai 2018.

Kuhusu familia ya Oliech:

1. Steve Okumu Oliech

Alikuwa mwanambee katika familia. Aliwahi kuchezea Harambee Stars, Gor Mahia na AFC Leopards akiwa mshambuliaji. Alihamis Amerika baada ya kupata ufadhili wa soka na safari yake ikadhaminiwa na kocha Bob Oyugi. Aliaga dunia mnamo 2002 baada ya kuhusika kwenye ajali ya barabara mjini Rhode Island akiwa na umri wa miaka 26. Alifariki mwaka mmoja baada ya kifo cha baba mzazi.

2. Nixon Onywanda

Amekuwa msemaji mkuu wa familia na kiongozi wa masuala mbalimbali ya familia. Ndiye alikuwa meneja wa Dennis Oliech.

3. Andrew ‘Apache’ Oyombe

Alikuwa sehemu ya kikosi cha Harambee Stars kilichoshiriki fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo 2004 nchini Tunisia. Aliwahi kuvalia jezi za Gor Mahia na Tusker kisha kuhamia Uswidi kusakata soka ya kimataifa kabla ya kustaafu.

4. Kennedy Oliech

Ni mfumaji na nahodha wa zamani wa Gor Mahia. Kwa sasa amestaafu soka. Aliwahi kuwania urais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) mnamo 2016 na kupoteza. Kwa sasa yuko Ujerumani anakojifunza masuala ya ukocha. Anamiliki Wakfu wa Ken Oliech ambao unapania kukuza talanta za wanasoka chipukizi.

5. Dennis Oliech

Alianza kucheza soka akivalia jezi za Dagoreti Santos kabla ya kuingia katika sajili rasmi ya Mathare United. Aliwajibishwa na Harambee Stars kwa mara ya kwanza mnamo 2002 kwenye fainali za Cecafa Senior Challenge alikotegemewa sana kama mchezaji wa akiba. Alianza kupiga soka kitaaluma zaidi mnamo 2003 baada ya kuhamia Al-Arabi ya Qatar.

Mnamo 2004, alipata ofay a kubadilisha uraia kutoka taifa la Qatar na akaitupilia mbali. Akiwa na umri wa miaka 19, Dennis Oliech aliorodheshwa na mojawapo ya magazeti ya Uingereza kuwa miongoni mwa wanasoka chipukizi wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani.

Aliwahi kuchezea Al-Arabi (2003-2005), Nantes (2005-2007), Auxerre (2007-12), Ajaccio (2013-2015) na Dubai CSC (2015) kabla ya kurejea Kenya kuvalia jezi za Gor Mahia kwa muda mfupi mnamo 2019.