Habari Mseto

KFS lawamani kulemewa kuimarisha huduma za feri Mtongwe

April 30th, 2018 2 min read

Na MOHAMED AHMED

WAKAZI wa Mtongwe wamelilaumu Shirika la Huduma za Feri (KFS) kwa kushindwa kudumisha huduma za feri katika kivuko cha Mtongwe.

Kwa miezi miwili sasa, wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakitumia kivuko cha Likoni baada ya usimamizi wa KFS kuondoa feri ya Mv Likoni ambayo ilikuwa ikihudumu katika kivuko hicho.

Huduma hizo zilirudishwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi mwaka jana, baada ya kusimamishwa kwa miaka mitano.

Feri ya Mv Likoni ambayo ilikuwa imewekwa kuhudumu kivukoni hapo imekuwa ikihudumu katika kivuko cha Likoni kwa miezi hiyo miwili sasa baada ya feri ya Mv Jambo kuharibika.

Aidha, hata baada ya feri hiyo ya Mv Jambo kurekebishwa, feri hiyo ya Mv Likoni bado haijarudishwa.

Jumapili walidai kubaguliwa kufuatia kuondolewa kwa huduma hizo katika kivuko cha Mtongwe.

“Kivuko cha Likoni kina feri tano na sisi hatuna hata moja. Tunatumia pesa nyingi tukitumia kivuko cha Likoni lakini hawajali hilo,” akasema mmoja wa wakazi, Bw Michael Omondi.

Mkazi mwengine, Bakari Mweza alililaumu shirika hilo kwa kuharibu biashara zao kwa sababu ya kutostawisha huduma hizo.

Inasemekana usimamizi wa Kenya Ferry hautaki kuondoa feri yoyote Likoni kwa hofu ya kuwepo kwa feri tatu kuukuu.

Akizungumza na Taifa Leo afisa wa mawasiliano wa KFS Bi Elizabeth Wachira alisema kuwa feri ya Mv Likoni haijarudishwa kwa sababu ya kuharibika kwa feri ya Mv Kwale.

“Mipango iliokuwa ni muda Mv Kwale itamalizwa kurekebishwa ndipo Mv Likoni itarudishwa katika kivuko cha Mtongwe. Kwa sasa tunasubiri propela ya feri ya Mv Kwale,” akasema Bi Wachira.

Feri ya Mv Kwale imekuwa haihudumu kwa takriban miezi tano sasa.

Feri tano Mv Likoni, Mv Nyayo, Mv Harambee, Mv Kilindini na ile mpya ya Mv Jambo ndio zimekuwa zikihudumu katika kivuko hicho cha Likoni.

Feri hizo za Mv Nyayo, Mv Kilindini na Mv Harambee ambazo zilinunuliwa mnamo mwaka 1990 zimekuwa na wakati mgumu kuhudumu kivukoni hapo na kusaidia kupunguza msongamano wa magari na watu.

Zaidi ya watu 330, 000 na magari 6, 000 hutumia kivuko hicho cha Likoni kila siku.