KFS yawahakikishia wakazi huduma za feri zitarejea mwaka 2022

KFS yawahakikishia wakazi huduma za feri zitarejea mwaka 2022

Na WINNIE ATIENO

Huduma za feri ambazo zilisitishwa miezi mitatu iliyopita, zitarajea baada ya serikali kumaliza ukarabati wa sehemu ya daraja ambalo liliharibika Januari.

KPA imekuwa ikikarabati daraja hilo kwa kima cha Sh398 milioni baada ya sehemu kuharibika mara mbili hali iliyohatarisha maisha ya wasafiri.

Kamati ya Bunge Kuhusu Uwekezaji imekuwa ikichunguza ubadhirifu wa fedha kwenye ukarabati huo ambao wanakandarasi wamekashifiwa kwa kuzembea na kufanya kazi duni.

Mkurugenzi wa Huduma za Feri Nchini (KFS) Bakari Gowa, Jumamosi alitetea ukarabati huo ambao umechukua muda mrefu, akisema kwa sasa mchakato wa kutoa zabuni unaendelea na mwakani huduma za feri zitarajelewa.

“Tunatarajia huduma zinarejelewa mnamo Januari. Vyuma ambavyo ni sehemu ya daraja hilo vilikuwa vimezibwa na maji na sasa kiwango cha maji kinaelekea kupungua ili vichomwe.Kwa sasa ukarabati wa sehemu zote unaendelea vizuri na haja kuu ni kuhakikisha shughuli za usafiri zikirejelewa zitakuwa salama,” akasema Bw Gowa.

Mwanzoni, Shirika la Huduma za Feri (KFS) ambalo sasa liko chini ya KPA, lilitekeleza ukarabati kwenye daraja hilo ambalo linapakana na Bara Hindi.

“Kwa sasa huduma za usafiri wa feri haziwezi kurejelewa kwa kuwa hiyo itakuwa kuhatarisha maisha ya wasafiri. Ni vyema ukarabati wa daraja unaoendelea ukamilike pande zote,” akaongeza.

Hapo awali huduma za feri ambazo hutumiwa na watu 3,000 kila siku ziliendelea kwa muda wa miezi 19 baada ya uzinduzi ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

“Hatukuwa na shida wakati huo na usafiri uliendelea vizuri. Hata hivyo, mnamo Septemba, tulifanya uchunguzi wetu na tukapata kulikuwa na uharibifu ambao ungehatarisha maisha ya raia,” akaongeza.

Mwenyekiti wa PIC Abdulswamad Nassir na wanachama wa kundi hilo wakiwemo Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Nyeri Rahab Mwikali, Mishi Mboko (Likoni), Teddy Mwambire (Ganze) Paul Katana (Kaloleni) na Mathias Robi wa Kuria Mashariki walitaka KPA iharakishe ukarabati huo.

“Walifanya kazi mbovu na kutumia vifaa vya kiwango cha chini. Muda wa miezi 19 ni mchache sana kwa daraja ambalo lilitengenezwa hapo awali kuharibika. Lengo la wanakandarasi hawa ni kukula pesa,” akasema Bw Ashid Kassim, mbunge wa Marsabit Magharibi.

“Ninashughulishwa sana na suala hili kwa sababu mradi huu ungekamilika zamani na hata muda huu ambao umesongeshwa hata hawatamaliza kazi hii. Huu mradi umekwama kwa muda mwingi na tunafaa kuwahakikishia wakazi wa Pwani kuwa usafiri utarejelewa kama zamani,” akaongeza.

Kauli yake iliungwa mkono na Bw Katana ambaye alitaka KPA itoe stakabadhi zote za utoaji zabuni na gharama iliyotumika kwa ukarabati wa mwanzo ndipo bunge ibaini iwapo kulikuwa na ubadhirifu wa pesa.

You can share this post!

Kampuni yafuta shoo ya Olomide jijini

Majonzi zaidi ya 30 wakihofiwa kufariki mtoni

T L