Habari za Kitaifa

Khalwale afanya tambiko kwa fahali kumuua mfanyakazi

January 29th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

SENETA wa Kakamega Boni Khalwale, amefanya tambiko la kumchinja ng’ombe aliyesababisha kifo cha mchungaji wa mifugo nyumbani kwake Malinya, eneobunge la Ikolomani, Kaunti ya Kakamega.

Katika video aliyopakia kwenye ukurasa wa X (zamani Twitter), seneta huyu alilaani hatua ya ng’ombe kusababisha mauti kinyume na tamaduni za jamii hiyo.

Mkononi mwake akiwa na mkuki pamoja na mshale aliotumika kutekeleza tambiko hiyo, Bw Khalwale alitoa kauli kadhaa kabla ya kumaliza kizazi cha ‘Inasio’.

“Mtu ndiye humchinja ng’ombe. Ng’ombe hafai kutekeleza maafa kwa mwanadamu. Inasio, umefanya makosa, rudi mahali ambapo ulitoka,” Bw Khalwale alisikika akisema kwenye video hiyo.

Pia, alipakia ujumbe uliondamana na video hiyo, ikiwa ni ishara ya kughadhabishwa na kitendo cha ng’ombe huyo ambaye wakati mwingi huhusishwa kwenye mchezo wa vita vya fahali almaarufu ‘bull fighting’, Kaunti ya Kakamega.

“Kuzingatia utamaduni wetu, kwa kumuua mlezi wake, ng’ombe huyu bingwa kwa jina Inasio anakutana na kifo chake kwa nguvu ya Mkuki wangu,” alisema mwanasiasa huyo.

Inasio alimuua Bw Kizito Moi Amukune,46, ambaye amekuwa akimhudumia kwa muda wa miaka 24.

Kimila, mwanamume kapera asiye na watoto ndiye hutwikwa jukumu la kuwafunza fahali wa kupigana.