Habari

Khalwale ataka Kanisa limuombee Ruto

March 10th, 2020 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

ALIYEKUWA Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amelitaka Kanisa kumuombea Naibu Rais William Ruto akidai uhai wake uko katika hatari.

Khalwale anadai wapo watu ambao wanafanya kila hila kuhakikisha Ruto hafaulu kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ifikapo mwaka 2022 kwa vyovyote vile.

Akizungumza akiwa Ikolomani katika Kanisa, mwanasiasa huyo alilaumu maafisa wa polisi kwa kutowakamata baadhi ya viongozi wanaotoa kauli za kuweka uhai wa Ruto hatarini.

“Tumewasikia watu wengi wakiwemo aliyekuwa naibu mwenyekiti wa Jubilee David Murathe akisema Ruto jina lake halitokuwa katika karatasi ya kura mwaka 2022 na Katibu Mkuu wa Cotu Francis Atwoli kusema Ruto huenda asikuwepo naye Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i akiagiza maafisa wa usalama wasusie hafla za Ruto; hizi kauli zinamaanisha nini?” akauliza Khalwale.

Khalwale anasema ikiwa serikali imeshindwa kuwakamata wanasiasa wanaotishia uhai wa Dkt Ruto, basi Kanisa halina budi ila kumwombea Ruto asikutwe na chochote kibaya.

“Kauli zinazotolewa na wabaya wa Ruto si mzaha. Je, kina Saitoti na Nkaisery walikufa namna gani? Hatuwezi tukachukulia matamshi hayo kimzaha,” akaongeza.