Khalwale, Echesa waahidi kupiga jeki azma ya Malala

Khalwale, Echesa waahidi kupiga jeki azma ya Malala

NA SHAABAN MAKOKHA

SENETA wa Kakamega Cleophas Malala na aliyekuwa seneta wa kaunti hiyo Boni Khalwale, hatimaye wamekubali kuzika tofauti zao na kushirikiana ili washinde viti katika uchaguzi mkuu ujao.

Wanasiasa hao wawili walianika tofauti zao katika mkutano wa Kenya Kwanza eneo la Matungu mwezi Juni, ambapo Bw Malala alimlaumu Dkt Khalwale kwa kumpigia debe mgombeaji wa ugavana Kakamega, Bw Fernandes Barasa wa ODM.

Hata hivyo, Jumamosi walitangaza kushirikiana, Bw Malala alipozindua manifesto yake katika uga wa Mumias Complex, hafla ambayo ilihudhuriwa na kinara wa ANC, Bw Musalia Mudavadi pamoja na wanasiasa kadhaa wanaomuunga Dkt Ruto.

“Hatutakubali siasa isababishe mgawanyiko kati ya watu wetu. Tuliagana na Bw Malala kuwa tutaendesha kampeni za pamoja kwa sababu tukitengana, bila shaka tutashindwa,” akasema Dkt Khalwale.

Naye Bw Rashid Echesa ambaye anawania kiti cha ubunge wa Mumias Magharibi, aliahidi kuwa wafuasi wake watamuunga mkono Bw Malala.

“Kwa kuzindua manifesto yako hapa kwa ardhi ya jamii ya Wanga na ufalme wa Nabongo Mumia, umeonyesha kuwa unawajali watu wa Mumias. Nitakutafutia kura upande huu kuhakikisha kuwa unashinda ugavana,” akasema Bw Echesa.

Mabw Echesa na Malala wamekuwa na uhasama mkubwa kisiasa ila kuungana kwa Dkt Ruto na Bw Mudavadi kumeonekana kuwaunganisha. Awali Bw Echesa alikuwa akimuunga mkono mwaniaji wa ugavana wa ODM Fernandes Barasa.

Bw Malala aliahidi kuimarisha uchumi wa kaunti hiyo kwenye manifesto yake na pia kutodhalilisha naibu gavana akichukua usukani.

Ingawa ameshutumiwa kwa kupinga kufufuliwa kwa kiwanda cha sukari cha Mumias, Bw Malala aliahidi kuwa atashirikiana na mwekezaji yeyote ambaye ataonyesha nia nzuri ya kuhakikisha kiwanda hicho kinarejelea shughuli zake.

“Sikupinga kufufuliwa kwa kiwanda cha Mumias jinsi ambavyo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakidai. Kile nilipinga ni kuuzwa kwa mali ya kiwanda hicho na baadhi ya wanasiasa,” akasema Bw Malala.

Kati ya masuala mengine kwenye manifesto yake aliyoahidi kutekeleza ni kuongeza kiwango cha basari kinachotolewa kwa wanafunzi na kubuni nafasi za ajira.

Mbunge wa Soy Caleb Kositany aliahidi kuwa serikali ya Kenya Kwanza itatoa kipaumbele kwa ufufuaji wa viwanda vya sukari Magharibi mwa nchi ili kubuni nafasi za ajira.

“Tunaheshimu jamii ya Waluhya na tutatimiza ahadi zote tulizotoa kwa Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula kwa kukubali kufanya kazi na Naibu Rais Dkt William Ruto,” akasema Bw Kositany.

Kwa upande wake Bw Mudavadi alisisitiza kuwa Bw Malala na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja watakuwa debeni licha ya kile alichodai kuhangaishwa na serikali.

  • Tags

You can share this post!

Omurwa ajiunga na Sektzia Ness Ziona FC ya Israel

Joho ndiye chanzo cha shida zetu – Omar

T L