Habari

Khalwale sasa mali rasmi ya Jubilee

May 17th, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU na SHABAN MAKOKHA

ALIYEKUWA Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, ametangaza kuhama rasmi kutoka chama cha Ford-Kenya na kujiunga na Chama cha Jubilee (JP), akilalamikia “vitisho” kutoka kwa uongozi wake.

Dkt Khalwale, ambaye amekuwa akihudumu kama Naibu Kiongozi wa chama hicho, alikuwa ametakiwa kufika mbele ya kamati yake ya nidhamu Alhamisi wiki ijayo, kujibu tuhuma za kuasi kanuni zake.

Kiongozi huyo amekuwa akimpigia debe Naibu Rais William Ruto, akishikilia kuwa atamuunga mkono kuwania urais mnamo 2022. Hii ni licha ya chama hicho kutotoa msimamo wake kuhusu yule kitamuunga mkono.

Akihutubu nyumbani kwake katika kijiji cha Malinya, Kaunti Ndogo ya Ikolomani, Khalwale alisema alichukua hatua hiyo, baada ya kamati hiyo kutishia kumwondoa kutoka nafasi yake.

“Sitaenda kuaibishwa kwa kisingizio cha nidhamu. Ninahangaishwa kwa kuitafutia nafasi jamii ya Waluhya katika serikali ijayo,” akasema.

Akaongeza: “Nimewaita nyote nyumbani kwangu ili Kenya iweze kufahamu ninakotoka. Nipo hapa kutangaza rasmi kuwa nimehama Ford-Kenya na kujiunga na Jubilee.”

Kujibu tuhuma

Dkt Ruto pia alikuwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria. Chama kilimwandikia barua kwa mara ya kwanza mnamo Machi 26, kikimtaka kujibu tuhuma za kukiuka msimamo wake, lakini akakataa kuijibu.

Aliandikiwa barua ya pili mnamo Jumatatu, ambapo alipewa hadi Jumanne ijayo kujibu tuhuma hizo na kufika mbele ya kamati yake ya nidhamu mnamo Alhamisi.

“Kukosa kuijibu barua hii huenda kukaifanya kamati kukuchukulia hatua, mojawapo ikiwa ni faini,” ikamwonya barua hiyo.

Ijumaa, Dkt Khalwale pia alitangaza kuwania ugavana katika kaunti hiyo mnamo 2022.

Kwa upande wake, Dkt Ruto alisema kuwa nia yake ni kuendeleza umoja wa nchi.

“Nipo hapa kumpokea Dkt Khalwale ili kuungana na viongozi wengine ambao hawataki kuendeleza siasa za kikabila ambazo huzua chuki. Mnamo 2013, niliwaomba viongozi wenzangu kutoka vyama vingine kuvivunja na kubuni chama cha umoja wa kitaifa lakini wakakataa. Leo (nawakumbusha kuwa, ikiwa hawataungana, watashindwa vibaya hata kuliko 2013,” akasema.