Khan ajiondoa katika kesi ya Gicheru ICC

Khan ajiondoa katika kesi ya Gicheru ICC

Na VALENTINE OBARA

ALIYEKUWA wakili wa Naibu Rais, William Ruto katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Bw Karim Khan, amejiondoa rasmi kuwa kiongozi wa mashtaka katika kesi ya wakili Paul Gicheru.

Bw Khan aliapishwa mapema Juni kuchukua nafasi ya aliyekuwa mwendesha mashtaka ICC, Bi Fatou Bensouda ambaye alikamilisha kipindi chake cha kusimamia idara hiyo.

Kwenye taarifa Jaji Reine Alapini-Gansou anayesikiliza kesi ya Bw Gicheru alisema mahakama ilifahamishwa kuwa kesi hiyo sasa itaongozwa na naibu kiongozi wa mashtaka, Bw James Stewart.

“Mnamo Juni 28, Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka iliarifu mahakama hii kwamba, kiongozi wa sasa wa mahakama amejiondoa katika kesi hii. Ilieleza kuwa naibu kiongozi wa mashtaka ndiye atachukua mamlaka yote ya kiongozi wa mashtaka katika kesi hii,” akasema jaji huyo.

Kwa msingi huu, Bw Khan hatakubaliwa kuona stakabadhi zozote zinazohusu kesi hiyo ambazo hazitachapishwa kwa umma, wala hatakubaliwa kuhusika katika majadiliano wala maamuzi yoyote au usimamizi unaohusiana na kesi hiyo.

Bw Gicheru alijisalimisha ICC mwishoni mwa mwaka uliopita akikumbwa na madai ya kuhusika katika njama ya kushawishi mashahidi wajiondoe kwa kesi ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 iliyomwandama Dkt Ruto.

You can share this post!

Mawakili wakosoa hatua ya kushtaki rais

Tuju sasa awataka wanachama waasi wahame Jubilee